HALIMA MDEE na wenzake 18 waliovuliwa uanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Kamati Kuu ya chama hicho wiki iliyopita, leo Jumanne, Desemba Mosi, 2020, wamesema watatafuta ufumbuzi wa tatizo hilo kwa kukata rufaa kwa Baraza Kuu la chama hicho.
Ameyasema hayo akiwa na wenzake wakati akizungumza na waandishi wa habari katika hoteli ya Regency jijini Dar es Salaam ambako amesisitiza kwamba wataendelea kuwa wanachama wa Chadema kwa kuwa wameshiriki kwa kiwango kikubwa katika kukijenga hadi kilipofikia sasa.
"Licha ya kwamba tumevuliwa uanachama wa Chadema, leo tumevaa kombati. Tutaendelea kuwa wanachama wa hiyari wa Chadema, wakati tukishughulikia taratibu za kikatiba ndani ya chama," Mdee amesisitiza kuonyesha kwamba yeye na wenzake wanataka ufumbuzi au suluhu vipatikane kupitia michakato ya chama hicho.
Mdee aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha) na viongozi wengine wanawake wa ngazi za juu wa Chadema kabla ya kuvuliwa uanachama, waliapishwa hivi karibuni na Spika wa Bunge, Job Ndugai, kuwa wabunge wa viti maalum wa chama hicho kwa njia ambazo uongozi wa chama hicho umesema haukufuata njia sahihi na kwamba haukuhusika kwa vyovyote katika kuwateua.