JENGO la ghorofa linalofahamika kama House of Wonders au Palace of Wonders (Beit Al Ajaib) lililopo Stone Town, Zanzibar limeanguka huku baadhi ya watu waliokuwemo wakidaiwa kufukiwa na kifusi cha jengo hilo leo Ijumaa, Desemba 25, 2020.
Jengo hilo linalotazamana na Bustani ya Forodhani ndilo jengo kubwa na refu zaidi katika eneo la Stone Town na ni miongoni mwa majengo kongwe (ya kale) ambalo lilijengwa mwaka 1883 na baadaye kufanyiwa ukarabati miaka ya hivi karibuni.
Imeelezwa kuwa jengo hilo ambalo lipo pembezoni mwa Bahari ya Hindi katika Barabara ya Mizingani, limejengwa kati ya ya makumbusho ya kale ya Zanzibar ambalo pia limekuwa kielelezo kikubwa cha historia na tamaduni za watu wa Zanzibar na kukua kwa lugha ya Kiswahili.
House of Wonders lilikuwa miongoni mwa majengo sita ya Ikulu na makazi ya zamani ya Sultan wa pili wa Zanzibar, Barghash bin Said, enzi za ukoloni na biashara, karne ya 17.
House of Wonders kwa sasa lilikuwa limefungwa kutumika kutokana na sehemu kubwa ya jengo hilo kupasuka na kuharibika na kuanguka veranda mwaka 2012 kisha kuanguka paa lake mwaka 2015, hivyo kuharibu muundo, uimara na mwonekano wa jengo hilo ambapo makumbusho yake yalilazimika kuhamishiwa eneo jingine.
Global TV Online imemtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini, Magharibi, Alhaji Awadhi, kuzungumzia tukio hilo lakini bahati mbaya alikuwa na kazi nyingi na badala yake tumeongea na msaidizi wake ambaye amesisitiza tumtafute kamanda mwenyewe baadaye ili azungumze.
Tunaendelea kumtafuta Kamanda ili kupata taarifa Zaidi… endelea kuwa nasi.
Updates:
Mtu mmoja aokolewa na kukimbizwa hospitali, huku juhudi za kuwanasua wengine zikiendelea baada ya Jumba maarufu la Beit Al Ajaib lililokuwa likikarabatiwa lililopo mji Mkongwe visiwani Zanzibar kuanguka. Jumba hilo linakadiriwa kuwa na Ghorofa nne mpaka 5.
Rais wa Zanzibar, Dr. Hussein Ali Hassan Mwinyi, amefika eneo la Forodhani ambapo jengo la Bait-Al Jaib, limeporomoka na kusema kwa sasa Serikali inafanya juhudi za kuokoa maisha ya watu watatu wanaodhaniwa wamekwama kwenye kifusi cha jengo hilo.
Source