Saturday, November 28, 2020

TAMWA YAONESHA NJIA YA KUMALIZA UDHALILISHAJI ZANZIBAR

Baadhi ya wanafunzi kutoka shule mbalimbali kisiwani Pemba wakionesha bango lenye ujumbe wa kukataa kupinga vitendo vya udhalilishaji katika viwanja vya Gombani ya kale Pemba.
***

Mkuu wa Wilaya ya Chake Chake Mkoa wa kusini Pemba  Rashid Khadid Rashid ameelezea kutoridhishwa na baadhi ya watendaji wa vyombo vya mahakama, polisi pamoja na wanaharakati wanaoshiriki kufanya suluhu dhidi ya kesi za udhalilishaji na kusema hali hiyo inachangia kukwamisha juhudi za serikali za kuyatokomeza matendo hayo.

Akizungumza kwenye maadhimisho ya siku kumi na sita za kupinga ukatili wa kijinsia katika viwanja wa Gombani kisiwani Pemba yaliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA Zanzibar).

Mkuu huyo wa Wilaya amezitaka kamati za kupinga udhalilishaji za wilaya kushirikiana na Ofisi ya Mufti kutoa elimu ya ndoa kwa wanandoa  pamoja na sehemu zenye mikusanyiko ya watu ikiwemo maskulini.

Amesema kesi nyingi za udhalilishaji zinashindwa kupatiwa ufumbuzi wa haraka kutokana na kuwepo na baadhi ya watumishi wa vyombo vinavyosomamia sheria kukosa uadilifu.

"Miongoni mwa mambo yanayochangia kesi hizi ziendelee kutokea ni uwepo wa baadhi ya watumishi ambao sio waadilifu wanaoshiriki kufanya suluhu, pamoja na hukumu ndogo zinazotolewa dhidi ya watuhumiwa,"alisema.

Akizungumzia kuhusu mwenendo wa matukio hayo Kisiwani Pemba amesema bado tatizo hilo lipo kwa kiwango kikubwa katika jamii licha ya matukio hayo kuanza kupungua ikilinganishwa na miaka iliyopita ikiwa ni kutokana na juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na wanaharakati mbalimbali wakiwemo TAMWA Zanzibar.

"Naomba niiambie hadhira hii kuwa vitendo vya udhalishaji bado ni tatizo kubwa na matukio haya yanaripotiwa kila siku katika jamii zetu, kwa mwaka huu hadi sasa tuna  kesi 218 ambazo zinafanyiwa kazi ktika ngazi mbalimbali ambapo kwa wilaya ya Wete ni 57, Micheweni 30, Chake Chake 84, na Mkoani 47 ambapo kesi za ubakaji ndizo zinazoongoza kwa wingi katika kesi hizi." alisema.

Mratibu wa TAMWA Pemba Fat-hiya Mussa Said amesema lengo la kuandaliwa kwa mazoezi hayo ya hiari ya siku moja ni kubadilisha tabia hasa za vijana dhidi ya fikra potofu za kubaka na kudhalilisha kwa ujumla kupitia ufanyaji wa mazoezi.

"TAMWA Zanzibar kwa kuwa ni wadau wakubwa wa kupambana na udhalilishaji wa wanawake na watoto tumeamua kuadhimisha siku hii kwa kufanya mazoezi ya hiari ili kupaza sauti za wanyonge kupitia kampeni  ya siku 16 za  kuhamasisha  jamii  kubadili tabia juu ya ukatili wa mtoto wa kike.''

Katika hatua nyingien Mratibu huyo amesema, TAMWA itaendelea kushirikiana wadau mbali mbali, ili kuhakikisha wanawake na watoto wanaishi bila ya ukatili na udhalilishaji.

Akitoa salama za wanawake, Mkuu wa Idara ya wanawake Pemba, Mwanaisha Ali Massoud, alisema siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto wa kike ni muhimu kwa jamii, ili kutafakari namna ya kuyakinga makundi hayo dhidi ya ukatili.

Alisema, udhalilishaji na ukatili huathiri sana wanaofanyiwa ikiwa ni pamoja na kukatisha ndoto zao ziwe na kielimu au biashara kutokana athari zake.

Alisema, "njia rahisi ya kupambana na matendo hayo ni kwa jamii kuondoa muhali na kushirikiana na vyombo vya sheria ikiwa ni pamoja Polisi na mahakama."

Tatu Abdalla Msellem kutoka jumuiya ya Tumaini Jipya Pemba (TUJIPE)ametoa wito kwa taassi na idara za serikali kuongoeza ushirikiano na asasi za kiraia hasa suala la upatikanaji wa takwimu ili kufanikisha mapambano dhidi ya vitendo hivyo.

"Ili kufanikisha kupiga vita matendo hayo, wakati mwengine tunapoomba miradi huhitaji takwimu, ili kupata ithibati, lakini huwa vigumu, sasa lazima hili lionekane na liondolewe,''aliesema.

Awali kwenye mkutano huo ulinogeshwa na kikundi cha mazoezi cha Gombani, usomaji wa utenzi pamoja na mchezo wa kuigiza kutoka kundi cha 'Thesode' la Ngwachani wilaya ya Mkoani Pemba.

Maadhimisho ya siku kumi na sita za kupinga ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto huadhimishwa kila ifikapo tarehe 25 Novemba hadi tarehe 10 Desemba ya kila mwaka ambapo Ujumbe wa mwaka huu ni TUPINGE UKATILI WA KIJINSIA , MABADILIKO YAANZE NA MIMI. Sambamba na ujumbe maalum wa TAMWA ZNZ 'Fanya mazoezi zuia mihemuko: Muache mtoto wakike salama.


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...