Friday, November 27, 2020

Simulizi Mfungwa Aliyempora Askari Bunduki ‘SMG’





NJOMBE: Ni ujasiri ulioje? Kijana, Isaack Kawogo (24) ambaye alikuwa mfungwa, amefanya tukio lililowaacha wengi midomo wazi la kumpora Askari Magereza silaha aina ya SMG (SubMachine Gun) mkoani Iringa, kabla ya kuuawa kwa kupigwa risasi na Polisi baada ya kumjeruhi kaka yake, Andres Kawogo (61), UWAZI lina simulizi hii ya kutisha.

 

Kawogo alikuwa akimtuhumu ndugu yake huyo kuuza mashamba ya nyumbani kwao na kushindwa kumtoa gerezani. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, ACP Hamis Issah aliliambia UWAZI kuwa, tukio hilo la kupora silaha hiyo lilijiri Novemba 20, mwaka huu huko maeneo ya Chaugingi mjini Njombe.

 

Kamanda Issah alisema kuwa, Kawongo aliiba silaha na kuitumia kufanya uhalifu ambapo alifanya matukio kadhaa huko mkoani Iringa ikiwemo kumshambulia Askari kwa panga, hali iliyosababisha wafungwa wengine kutoroka. "Hii ni silaha ambayo Askari Magereza wanaitumia katika ulinzi wa wafungwa hao, sasa huyu kwa kuwa ni mhalifu, akawa anaitumia katika kufanya uhalifu," alisema Kamanda Issah.

 

Alisema kuwa, silaha hiyo ilikuwa na risasi kumi, lakini mpaka inachukuliwa mikononi kwa Kawogo, ilikuwa imebakiwa na risasi mbili pekee huku risasi nane zikitumika kufanya ualifu maeneo tofauti ikiwemo tukio hilo lililotokea mkoani Njombe la kumjeruhi kaka yake.

 

Alisema kuwa, licha ya juhudi kufanyika za kutaka kuokoa maisha ya Kawogo ili alieleze Jeshi la Polisi namna alivyoondoka na silaha, lakini ilishindikana kwa kuwa umauti ulimfika wakati akinyang'anywa silaha hiyo.



"Ukimnyang'anya askari silaha, namna pekee ya kuipata hiyo silaha ni kwa kutumia silaha hivyo wanapaswa kuwa makini," Kamanda Issah.

 

Kwa mujibu wa watu waliozungumzia tukio hilo ambalo limekuwa gumzo katika Mikoa ya Njombe na Iringa, si jambo la kawaida kutokea na kwamba ni hatari mno.

 

"Si jambo la kawaida kutokea, ila kuna uzembe fulani utakuwa umefanywa na askari, haiwezekeni askari aporwe silaha, tena SMG akiwa ameishikilia, hii ni hatari sana," alisema Emmanuel Sanga, mkazi wa mjini Njome.

 

Tukio kama hilo liliwahi kutokea mkoani Arusha ambapo mahabusu mmoja alimpora silaha aina ya SMG mmoja wa Askari Polisi katika Mahakama Kuu jijini Arusha na kutokomea nayo mtaani, jambo lililozua taharuki kubwa, kabla ya kusakwa na kunyang'anywa kisha sheria kuchukua mkondo wake.


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...