Sunday, November 29, 2020

Serikali yasisitiza uwepo wa miradi kwa wafugaji


Serikali imesema katika kuboresha na kuondoa migogoro ya wakulima na wafugaji katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Mkoa wa Morogoro, inasisitiza uwepo wa miradi ambayo itakuwa na manufaa makubwa kwa makundi yote mawili.


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amesema hayo katika Wilaya ya Mvomero, Morogoro alipotembelea ujenzi wa mradi wa kiwanda cha nyama katika Ranchi ya Nguru Hills na kubainisha kuwa mradi huo unaotarajia kukamilika mwezi Aprili mwaka 2021 utakuwa na manufaa makubwa kwa wafugaji na wakazi wa Morogoro.


"Tumekuja kuangalia shughuli zinazoendelea kutokana na kikao ambacho tulikuwa nacho katika ofisi ya katibu tawala wa mkoa na mkuu wa Mkoa wa Morogoro katika kuboresha shughuli za mifugo kwenye mkoa huo na kuondoa changamoto za migogoro ya wafugaji ambapo uongozi wa mkoa waliniambia juu ya mradi huu ambao utakuwa na msaada mkubwa sana kwa wakulima na wafugaji wa mkoa wa Morogoro na nchi kwa ujumla." Amesema Prof. Gabriel


Prof. Gabriel amebainisha kuwa mradi huo wa kipekee ambao mara baada ya kiwanda hicho kukamilika kitakuwa na uwezo wa kuchinja mbuzi zaidi ya 200 na ng'ombe zaidi ya 1,000 kwa siku, kumejengwa mabwawa makubwa ambayo yatakuwa yanakusanya maji yanayotoka kwenye machinjio, kisha kutibiwa kabla ya kutumika tena kwa shughuli za kilimo cha umwagiliaji.


"Mradi huu una jambo mahsusi kuliko mingine, maji haya ya mabwawa yatatumika kwa ajili ya umwagiliaji huu ni moja kati ya miradi ambapo wafugaji na wakulima watanufaika ili wote waone huu mradi ni wa kwao kwa ajili ya uchumi wetu." Ameongeza Prof. Gabriel


Aidha amesema mradi huo wenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 25, ambao unashirikisha wabia mbalimbali ukiwemo Mfuko wa Pesheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), ni azma ya serikali katika kuzidi kuboresha mazingira ya uwekezaji hapa nchini kwenye sekta mbalimbali ikiwemo Sekta ya Mifugo hivyo kuwataka wafugaji kuboresha mifugo yao kwa kufuga ng'ombe bora wa kisasa na kupitia miradi ya kunenepesha mifugo ili waweze kuuza mifugo yenye ubora katika viwanda vya kusindika mazao ya mifugo hapa nchini ili sekta izidi kukua na kuchangia pato la taifa kupitia uchumi wa viwanda.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...