Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila ameamuru watu sita kukamatwa na kufikishwa mahakamani kwa kughushi sahihi za watu waliofariki dunia kisha Serikali kuwalipa fidia ya Sh108 milioni katika eneo lenye mradi wa soko.
Chalamila amesema hivyo leo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Iyunga jijini hapa ambako kuliibuka mgogoro wa eneo la soko huku watuhumiwa hao wakidai ni mali yao.
"Hawa wazee walifika ofisini kwangu na kuandika barua ofisi ya Rais na Waziri Mkuu waidai fidia ya Sh 108 milioni huku halmashauri ikiwa imewalipa fidia ya Sh 17 milioni ambazo ni halali na walipisha eneo hilo "amesema.
Chalamila anasema baada ya kuwasikiliza malalamiko yao amelazimika kuchunguza kwa kina na kubaini kuwa watuhumiwa hao ni matapeli tayari walilipwa fidia na kwamba kiwanja hicho chenye mradi wa soko ni eneo la urithi wa Wazazi wao ambao walipewa bure na kiongozi wa kimila na hivyo kufanya utapeli kwa serikali.
Mmoja wa watuhumiwa hao, Philimon Chapanga amekiri mbele ya umati wa watu kuwa walilipwa Sh 17 milioni na kwamba hawajaridhishwa na kiwango hicho cha fedha kwa kuwa eneo hilo la mradi wa soko lilikuwa kwa ajili ya kilabu cha wazee kujiliwaza jioni.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Jiji la Mbeya, Amude Ng'wanidako amesema watuhumiwa hao walilipwa Sh17 milioni ikiwa ni fidia ya mradi wa soko ambalo kwa sasa ni mali ya serikali .
Amesema kimsingi madai hayo si ya kweli ni suala la kuihujumu Serikali kwa madai ya fidia Sh 108 milioni.
"Mgogoro huu ni wa miaka mingi baada ya kufualia nyaraka na kamati zilizoundwa kufuatilia nimebaini wahusika hawaidai halmashauri na kwamba eneo la soko ni mali ya Serikali," amesema.
Akizungumza katika mkutano huo, Nelson Mayena mzee wa mila aliyetoa eneo hilo (chifu Mayena) amesema lilitolewa bure kwa watuhumiwa na walijenga klabu cha wazee kwa ajili ya maongezi ya jioni na kwamba awali walikubaliana na Serikali kulipwa fidia na kupisha mradi wa soko.
Amesema mwaka 2010 walikabidhi eneo hilo kwa Serikali na kulipwa fidia ya Sh17milioni suala na madai mengine silielewi.