Wednesday, November 25, 2020

Dkt. Mpango Awaasa Madiwani Nchini Kusimamia Vizuri Matumizi Ya Fedha Za Miradi


 Na Benny Mwaipaja, Kigoma
WAZIRI wa Fedha na Mipango, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Buhigwe mkoani Kigoma, Dkt. Philip Isdor Mpango, ameyaagiza mabaraza ya Madiwani kote nchini, kuhakikisha kuwa fedha za miradi zinazotumwa na Serikali katika maeneo yao zinasimamiwa vizuri ili kuleta tija na maendeleo ya jamii

Dkt. Mpango ametoa rai hiyo katika kata ya Mnanila mkoani Kigoma, wakati akiwashukuru wananchi kwa kumchagua kwa kura za kishindo, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na yeye binafsi wakati wa Uchaguzi Mkuu uliofanyika hivi karibuni.

Alionya kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua kali kwa watumishi wa umma watakaohusika kwa namna yoyote ile kujihusisha na vitendo vya ufisadi, ubadhirifu wa fedha za umma, rushwa na uzembe utakaoisababishia Serikali hasara.

"Hao mafisadi na wabadhirifu wa fedha za umma nawaonea huruma kwa sababu kisu nimepewa mwenyewe na Waziri wa Fedha hana mipaka, popote ilipo fedha na mali ya umma, akawapo mwizi, mbadhirifu, huyo ni halali yangu" alisema Dkt. Mpango.

Mishahara ya Watumishi wa Umma

Dkt. Mpango aliahidi kuwa Wizara yake imejipanga kutekeleza ahadi iliyotolewa na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli, kuhusu kuboresha maslahi ya watumishi wa umma ikiwemo nyongeza ya mishahara yao ili kuboresha na kukuza kipato chao.

"Kwahiyo lazima tufanyekazi ya kukusanya mapato na kutumia fedha vizuri ili watumishi hawa wanaohangaika kila siku na walau wapate kamshahara ambako kanasaidia zaidi" alisisitiza Dkt. Mpango.

Masuala ya Kipaumbele Jimboni Buhigwe

Dkt. Mpango aliwaahidi wakazi wa Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma, kwamba atatekeleza ahadi zote alizozitoa wakati wa kampeni na zile zilizoko kwenye Ilani ya CCM, lakini kwa kuanza ameyapa kipaumbele masuala mawili ambayo ni Ujenzi wa Barabara yenye urefu wa kilometa 2 inayoelekea kwenye Hospitali ya Misheni ya Heri pamoja na kutatua changamoto sugu ya maji katika tarafa ya Manyovu.

"Katibu Tawala wa Wilaya ya Buhigwe, Bw. Peter Masinde, kawaambie Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini TARURA, kwamba, nataka kuona barabara ya Manyovu hadi Hospitali ya Misheni-Heri inapitika wakati wote, wakati tunatafuta lami ya kujenga kipande hicho cha barabara cha kilometa mbili!" aliongeza Dkt. Mpango.

Kuhusu Sekta ya Maji, Dkt. Mpango alieleza kuwa katika mkataba wa ujenzi wa mradi wa barabara ya Kigoma- Buhigwe hadi Kasulu kuna kipengele cha mkandarasi kutakiwa kusambaza maji katika eneo la Manyovu na kwamba hatua hiyo itapunguza kero ya maji hususan kwa akina mama na watoto.

Awataka wana Kigoma kuchangamkia fursa mbalimbali

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, aliwataka wakazi wa Jimbo la Buhigwe na Mkoa wa Kigoma kwa ujumla, kuchangamkia fursa ya ujenzi wa meli mbili mpya pamoja na meli nyingine mbili za MT Sangara na MV Liemba zitakazo karabatiwa na kufanya safari zake katika Ziwa Tanganyika, ili kukuza biashara na kujipatia kipato.

"Serikali itajenga meli mpya mbili moja ikiwa na uwezo wa kubeba abiria 600 na mizigo tani 400 na meli nyingine itakuwa ya mizigo yenye uwezo wa kubeba tani 4,000 na pia tutakarabati meli ya kubeba mafuta MT Sangara na kukarabati meli nyingine ya MV Liemba, ambazo zitatumika kuimarisha usafiri wa abiria na mizigo kati ya Tanzania na nchi jirani" Alifafanua Dkt. Mpango.

Awataka wananchi wajenge utamaduni wa kuweka fedha zao Benki

Katika hatua nyingine Dkt. Mpango amewahimiza wananchi wa Wilaya ya Buhigwe, kujenga tabia ya kuhifadhi fedha zao benki kwa ajili ya usalama wa fedha zao na kuwezesha uwepo wa mzunguko mzuri wa fedha.

Alisema kuwa ameanza kuzishawishi Taasisi za Fedha hususan mabenki kujenga matawi yao ya Benki katika Wilaya ya Buhigwe lakini changamoto kubwa iliyo ainishwa na taasisi hizo ni kwamba wananchi wa wilaya hiyo hawana utamaduni wa kuweka akiba zao benki.

Kukuza Sekta za Kilimo, Mifugo, Uvuvi na Utalii

Dkt. Mpango, aliwataka wakazi wa Wilaya ya Buhigwe kuchangamkia fursa ya kilimo cha mazao ya kimkakati ikiwemo kahawa, michikichi, maparachichi, mkwa, mbogamboga na tangawizi ili kufaidi soko la kitaifa na kimataifa katika nchi ya Burundi.

Alisisitiza pia ufugaji wa kisasa na wenye tija pamoja na kuwashauri wananchi kuanzisha ranchi za kufuga wanyamapori pamoja na kuanzisha utalii wa kiutamaduni ili kukuza kipato chao na kuondokana na umasikini.

Serikali kuondoa kodi zenye kero kwa wajasiliamali

Dkt. Mpango aliahidi kuwa katika kukuza Sekta Binafsi, ikiwemo masuala ya uwekezaji na biashara za wajasiliamali wadogo, Serikali itachambua na kuondoa kodi mbalimbali zinazokwaza Sekta Binafsi ili kuwezesha mazingira mazuri ya ufanyaji biashara, kukuza ajira na mitaji.

"Lazima tutoe kipaumbele kukuza ujasiliamali, kuwasaidia wafanyabiashara, wenye viwanda vidogo vidogo, watoa huduma, na tutakuwa na jicho tofauti kukuza sekta hizo kwa kuondoa kodi zinazowakandamiza" Alisisitiza Dkt. Mpango.

Mwisho


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...