Sunday, November 29, 2020

Chadema wapiga shangwe baada ya diwani wao wa pekee jijini Arusha kuapa


Licha ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuwa na diwani mmoja wa Kata ya Olorieni, Laurence Kombe katika Halmashauri ya Jiji la Arusha, haikuwazuia wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa chama hicho kujitokeza kwa wingi wakati na baada ya kuapishwa kumshangilia.


 Shughuli za kiapo zimefanyika leo Jumapili, Novemba 29, 2020 kwa madiwani 33 wa Kata 25 na wa Viti Maalumu wanane katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa mkoa na kuhudhuriwa na wafuasi wa vyama vya CCM, Chadema na ndugu na marafiki.


Matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2020 yamekua kinyume na matokeo ya mwaka 2015 ambayo Chadema ilipata ushindi wa madiwani 24 isipokua kata moja ya Kati pekee iliyoenda CCM.


Baada ya madiwani wote kuapa na kumchagua Meya wa Jiji hilo, Maxmillian Iranqhe na Naibu wake, Veronica Mwelange, vifijo na nderemo kutoka kwa wafuasi wa vyama hivyo viwili zilifunika viunga vya ofisi ya Mkuu wa Mkoa.


Jitihada za kuwatuliza wafuasi wanaodaiwa kuwa ni wa Chadema ili kumruhusu Mkurugenzi wa Jiji, Dk John Pima kuendelea na shughuli za kumkabidhi Meya gari atakalokua akilitumia kwa ajili ya shughuli za serikali, hazikufaulu na ndipo walipoamua kutoka nje ya uzio na kuondoka na diwani huyo kwenye msafara wa magari na pikipiki.


Mmoja wa wafuasi wa CCM ambaye jina lake halikupatikana mara moja alisikika akikejeli shamrashamra za hao wanaodaiwa ni wafuasi wa Chadema kuwa hazina maana kwa kuwa wana diwani mmoja pekee kati ya madiwani 33 hivyo hawakupaswa kushangilia.


Katibu wa CCM wilaya ya Arusha, Denis Mwita alisema wamewakabidhi madiwani halmashauri hiyo ili washirikiane na watumishi wa halmashauri hiyo kuwaletea wananchi maendeleo.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...