Thursday, November 5, 2020

Assad asema mabilioni yaliyokwama Lebanon ndiyo chanzo cha kuanguka uchumi wa Syria


Rais wa Syria Bashar al Assad amesema mabilioni ya dola yaliyohifadhiwa na raia wa nchi yake nchini Lebanon na kisha kuzuiwa wakati wa mzozo wa kifedha ndiyo sababu ya kudorora kwa uchumi wa Syria. 

Akuzungumza wakati alipotembelea maonesho ya biashara yanayoendelea nchini Syria, Assad amesema kiasi dola bilioni 20 hadi 42 za akiba iliyowekwa na raia wa nchi hiyo inaweza kuwa imepotea nchini Lebanon, kiwango ambacho kimechochea hali ngumu ya uchumi nchini mwake. 

Wafanyabiashara wa Syria wanasema masharti magumu ya kutoa fedha yaliyowekwa na Lebanon yamezuia mabilioni ya dola ambazo kabla zilitumika kuagiza mahitaji muhimu ikiwemo mafuta na bidhaa nyingine kwa ajili ya Syria. 

Kwa muda mrefu kampuni kubwa za Syria hukwepa vikwazo vilivyowekwa na mataifa ya magharibi kwa kutumia mfumo wa benki wa Lebanon kuagiza bidhaa zilizopigwa marufuku kwa kutumia njia ya barabara.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...