Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa nchi 50 zimeidhinisha mkataba wa Umoja wa Mataifa wa kupiga marufuku silaha za nyuklia na kuchochea kutekelezwa kwake katika muda wa siku 90.
Hatua hiyo inasifiwa na wanaharakati wa kupambana na matumizi ya nyuklia lakini inapingwa vikali na Marekani na mataifa mengine yenye ushawishi mkubwa wa nyuklia.
Hadi siku ya Ijumaa, mkataba huo ulikuwa na saini kutoka mataifa 49 na maafisa wa Umoja wa Mataifa wamesema Honduras imekuwa nchi 50 kuridhia mkataba huo.
Beatrice Fihn, mkurugenzi mtendaji wa kampeni ya kimataifa ya kukomesha silaha za nyuklia, amesema hatua hiyo imechukuwa muda wa miaka 75 tangu shambulizi la kutisha la nyuklia dhidi ya miji ya Hiroshima na Nagasaki na kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa ambao ulitoa kipaumbele kuzuia silaha za nyuklia.
Marekani imeyaandikia mataifa yaliotia saini mkataba huo na kusema serikali yake inaamini kuwa yalifanya ''kosa la kimkakati'' na kuyahimiza kubatilisha misimamo yao.