Mmoja wa wakosoaji wakubwa wa kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Franc
is amesema kauli yake ya hivi karibuni kuhusu wapenzi wa jinsia moja ni maoni binafsi ambayo hayastahili kuzingatiwa na Wakatoliki.
Kadinali Raymond Burke anayeonekana kuwa mhafidhina katika Kanisa Katoliki, ametoa tamko hilo siku chache baada ya Papa Francis kuonekana kuunga mkono wazo la kutambuliwa kisheria kwa watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja.
Kadinali Burke anasema pendekezo la Papa Francis la kutaka ndoa ya wapenzi wa jinsia moja kutambuliwa kisheria halijawashangaza wengi lakini maneno aliyotumia ndio yaliyowashangaza sana viongozi wa kidini na waumini wa Kanisa Katoliki.
Kadinali huyo ametaja matamshi ya Papa kama maoni ya kibinafsi na kwamba Kanisa katoliki na waumini wake hawatashurutishwa kutii msimamo wa kiongozi wa Kanisa hilo kuhusu suala la wapenzi wa jinsia moja.
Pia amesema viongozi wa kidini wa kanisa hilo wana jukumu la kutoa kile alichokitaja kama maelezo ya kina kuhusu suala hilo.
Kadinali Burke amesema imani rasmi ya kanisa Katoliki la Roma ni kuwa ndoa ya wapenzi wa jinsia moja hairuhisiwi na kwamba matamshi hayo ya papa yamewahuzunisha waumini wengi akidai kuwa matamshi ya papa hayaambatani na mafundisho ya Kanisa hilo.
"Watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja wana haki ya kuwa na familia,"alisema katika filamu, ambayo ilionyeshwa kwa mara ya kwanza siku ya Jumatano wiki hii."
"Ni watoto wa Mungu nawana haki ya kuwa na familia. Hakuna mtu anayestahili kutengwa ama kufanywa ajihisi mnyonge kwa kuamua kuwa katika uhusiano wa aina hiyo.
"Tunachopaswa kuunda ni sheria ya kutambua uhusiano wao ili kuwalinda kisheria."
Aliongeza kwamba "aliunga mkono wazo hilo", akiashiria nyakati alipokuwa Askofu Mkuu wa Buenos Aires, akisema japo alipinga ndoa ya wapenzi wa jinsia moja, aliunga mkono ulinzi wa kisheria kwa watu walio kwenye mahusiano ya kama hayo.
Filamu ya Francesco, inayoangazia maisha na kazi ya Papa Francis, ilionyeshwa kama sehemu ya Tamasha la Filamu la Roma.