Thursday, November 8, 2018

Mwandishi wa Kenya na Afrika kusini waachiwa huru


Kufuatia kusambaa kwa taarifa kuhusu Wawakilishi wawili wa kamati ya kimataifa ya kuwalinda waandishi wa habari CPJ waliokuwa wamekamatwa nchini Tanzania wameachiwa huru kwa mujibu wa Taarifa kutoka serikali ya Afrika Kusini.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kuchapishwa kwenye tovuti ya CPJ, afisa mmoja aliyejitambulisha kuwa ni mfanyakazi wa Idara ya Uhamiaji aliwakamata wafanyakazi hao wawili wa CPJ Angela Quintal na Muthoki Mumo, katika hotel waliyofikia jijini Dar es Salaam ambapo walikagua vitu walivyokuwa navyo na baadae kuchukua pasi zao za kusafiria.

Taarifa hiyo ilidai wafanyakazi hao ambao wamekuja nchini kwa masuala ya kikazi, inaelezwa kuwa waliondolewa hotelini na kupelekwa sehemu wasioijua.

Mkurugenzi mtendaji wa CPJ Joel Simon awali alisema walikuwa na wasiwasi na usalama wa wafanyakazi wao huku wakidai kuwa waliingia Tanzania ki uhalali.

Alitoa wito kwa mamlaka nchini Tanzania kuwaachia na kuwarejeshea pasi zao za kusafiria.

"Ni jambo la kutia wasiwasi mkubwa kuwa huenda simu ya Angela Quintal imetumiwa bila idhini yake. Hatujawasiliana na Angela Quintal au Muthoki Mumo tangu wakamatwe na tunaamini kuwa wote wanazuiliwa na mamlaka za Tanzania," Joel Simon aliandika kwenye Twitter.

Hata hivyo akizungumza kwa njia ya simu afisa habari wa Idara ya Uhamiaji nchini Tanzania Ali Mtanda amesema hana habari kuhusiana na taarifa hiyo na kwamba bado hazikuwa zimefika makao makuu na kutaka kupewa muda, ili kuweza kuthibitisha.

Baada ya taarifa hiyo msemaji mkuu wa serikali ya jamhuri ya muungano wa tanzania kupitia ukurasa wake wa twitter ameandika kuwa wanafatilia kujua sababu ya waandishi hao wa CPJ waliruhusiwa kuingia nchini na baadae kuhojiwa na uhamiaji na hatimaye kuachiwa huru.



Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...