Friday, November 9, 2018

KANGI LUGOLA AFYATUKA KUHUSU MASHOGA : SERIKALI HAITARUHUSU MWANADAMU KUBADILI MATUMIZI YA KIUNGO CHA KUTOLEA HAJA


Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amesema Serikali haitaruhusu hekalu la Mungu (Tanzania) kuchafuliwa na mambo yasiyokubalika ikiwemo ushoga.

Lugola ametoa kauli hiyo bungeni leo Ijumaa Novemba 9, 2018 wakati akitolea ufafanuzi kuhusu hoja iliyotolewa na Mbunge wa Konde (CCM) Khatibu Haji aliyoitoa wakati akichangia Mapendekezo ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo kwa mwaka wa fedha 2019/20.

Khatib amesema hivi karibuni kumezuka mjadala juu ya ndoa za jinsi moja na kwamba wamesikia sauti ya mawaziri akiwemo Lugola na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Augustine Mahiga.

"Katika kauli zao inaonekana kuna kamtego juu ya kukubiliana na kama kukinzana na jambo hili. Nataka niwaambie waheshimiwa iwe ni mtego ama bahati mbaya lakini sisi Tanzania hatutaingia katika mtego wa ushoga," amesema.

"Iwe mmetumwa ama kwa bahati mbaya Watanzania hatutakubali kuingia katika mtego huu ndoa ya jinsi mmoja. Tanzania ni Muungano wa nchi mbili Zanzibar ambayo Waislamu ni asilimia 99 kwa vyovyote vile hawakubali ushoga. Nawaambia nyoosheni kauli."

Amesema nchi haikubali ushoga na ndio msimamo wa Tanzania na kwamba anasikitika sana kwa sababu Tanzania ina utamaduni wake lakini kuna watu wanatumia kisingizio cha msaada kuwapeleka katika ubaradhuli (ushoga).

"Hili jambo ni baya na Watanzania hawataki kusikia hili. Nawaomba viongozi wangu mkae kimya kama hamliwezi. Leo tumezungumza hapa kuna chuma kule Liganga kwa nini tusitumie akili yetu mpaka tunafikia wakati wa kulainisha maneno, ohhh hatutawanyanyasa, tutawanyanyasa, hatutaki ushoga," amesema.

Kauli hiyo, ilimfanya Lugola kulazimika kutoa ufafanuzi kuwa hao mashoga ambao watu wanatumia viungo vyao kama binadamu na kwamba viungo vina kazi nyingine kwa mujibu wa uumbaji wa Mungu.

"Serikali haitaruhusu mwanadamu yeyote kubadili matumizi ya kiungo. Kubadili matumizi ya kiungo ambacho kimewekwa kwa ajili ya kutolea haja kitumike katika matumizi mengine ambayo mwenyezi Mungu hakukusudia," amesema.

"Serikali kwanza tuna sheria yetu ya kanuni ya adhabu ambayo inakataza ushoga, ambayo inazuia kubadilisha matumizi ya kiungo cha mwanadamu kwa hiyo asiseme kuwa Serikali inajichanganya ni maelekezo ambayo tunayatoa pengine vyombo vinaandika tofauti," amesema Lugola na kuongeza kuwa Tanzania ni hekalu la roho mtakatifu na mambo machafu hayakubaliki.

Kwa upande wake Khatib baada ya majibu hayo amesema kati ya taarifa nzuri ambazo ziliwahi kutolewa hiyo ni taarifa bora na kwamba alitegemea kauli ya kiume kama hiyo kutolewa na Kangi (Lugola).
Na Sharon Sauwa, Mwananchi 
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...