Thursday, August 16, 2018

Polisi wayanasa watu 8 kwa kuiba vyuma vya nguzo za umeme


Watu wanane wanaotuhumiwa kuhujumu uchumi Mkoani Morogoro wametiwa mbaroni na jeshi la Polisi kwa tuhuma za kufungua na kuiba vyuma vya nguzo za shirika la umeme nchini Tanesco.

Hayo yamebainishwa na kamanda wa Polisi Mkoani humo, Wilbroad Mutafungwa alipozungumza na waandishi wa habari na kusema kuwa wananchi wasiokuwa waaminifu wamediliki kukata vyuma vya shirika la umeme na kwenda kuuza kwa matumizi mbalimbali.

Kamanda Mutafungwa amebainisha matumizi ya vifaa hivyo kuwa ni pamoja na kutengenezea majembe ya kulimia ya mkono, milango pia kutengezea baadhi ya sehemu mbalimbali za mitambo.

Aidha ameongeza kuwa vifaa hivyo vinaigharimu Serikali pesa nyingi, hivyo kama jeshi la Polisi lenye mamlaka ya kulinda mali za umma litaendelea na misako mbalimbali ili kuwabaini wahalifu walioko maeneo tofauti tofauti.

"Operesheni hii ni endelevu itaendelea katika Mkoa wote wa Morogoro, hivyo nitoe rai kwa wananchi kama kuna mwenye vyuma kama hivi pengine ulivipata bila kujua tafadhari toa taarifa, lakini itakapokuwa umefikiwa na kikosi kazi kikiongozwa na watu wa shirika la umeme na jeshi la Polisi tukikukamata hautakuwa na nafasi tena ya kujitetea" aliongeza kamanda Mutafungwa.

Pia amewataka wananchi wa maeneo hayo kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo pindi wanapowabaini watu wenye nia ovu ya kuhumu uchumi nchi, hivyo rai yeyote mwenye vifaa hivyo avisalimisha ili kuendelea kuijenga nchi.

Kwa upande wake Afisa usalama wa Tanesco mkoani Morogoro Charles Ngwila amesema katika opesheni hiyo walioshirikiana na jeshi la polisi wamefanikiwa kuwakamata watu wanane na vyuma 117 katika maeneo ya Mang'ula na Pelege wilayani Kilombero.

Hivyo amewasihi wananchi wote wenye taarifa ya wahalifu watoe taarifa Tanesco na polisi ili wote wanaohusika na vitendo hivyo waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

Watuhumiwa hao nane walikamatwa Wilayani Ifakara wamefikishwa mahakamani kwenda kujibu mashtaka yanayowakabili ikiwa pamoja na uhujumu uchumi.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...