Saturday, August 18, 2018

KAULI YA WAZIRI KUHUSU WATANZANIA KUMILIKI LAINI MOJA TU YA SIMU YAZUA GUMZO

Kauli ya Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Atashasta Nditiye kuhusu udhibiti wa umiliki wa zaidi ya laini moja ya simu imezua mjadala huku watu wengi wakionyesha kutoelewa dhamira ya Serikali katika suala hilo.



Mjadala huo ulionekana kushika kasi mitandaoni watu wakihoji sababu za Serikali kufikia uamuzi huo, huku wengine wakitaka kujua hatima ya wanaomiliki laini zaidi ya moja.


Juzi, Nditiye aliripotiwa na kituo kimoja cha televisheni akieleza kuwa Serikali itaanza kudhibiti umiliki holela wa laini za simu kwa kutumia alama za vidole katika usajili, hivyo mtu atakayehitaji laini zaidi ya moja atalazimika kujazwa fomu ya kueleza kwa nini apatiwe.


Kwa mujibu wa Nditiye, katika kufanikisha udhibiti huo vitatumika vitambulisho vilivyotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida).


Utaratibu huo mpya utamtaka anayetaka kusajili laini zaidi ya moja atambuliwe na kampuni za simu na kujua kuwa tayari ana laini ya kwanza, hivyo lazima atajaza fomu maalumu kueleza kwa nini anataka ile ya pili.


Sambamba na hilo, Nditiye alisema kabla ya mwaka huu kuisha laini za simu zitaanza kuuzwa kwenye maduka rasmi na mtu anayesajili atachukuliwa alama za vidole na picha yake.


Akizungumza na Mwananchi jana, Waziri wa wizara hiyo, Isack Kamwele alithibitisha kuwepo kwa mpango huo ambao utaanza kwa Serikali kukaa na wataalamu wa Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA), kuangalia uwezekano wa kuwa na kanuni au sheria za kusimamia hilo. Alisema uamuzi wa kuelekeza matumizi ya laini moja ya simu unalenga kukabiliana na wizi na utapeli ambao umekuwa ukifanywa kwa njia ya simu.


"Baada ya kulivalia njuga suala la utapeli kwa njia ya simu, wale watu wanaotuma meseji ya kuelekeza watumiwe pesa walikamatwa na wengine wana laini zaidi ya 10, mwingine 30 sasa hii ni hatari," alisema Kamwele


Alisema baada ya utaratibu huo kupitishwa mtu mmoja atakuwa na namba ya simu kutoka mtandao mmoja na akiweza kuthibitisha matumizi ya namba ya simu ya mtandao mwingine ndipo atakapopewa.


Msemaji wa TCRA, Semu Mwakyanjala alipotakiwa kuzungumzia suala hilo alisema hajasikia na hivyo akataka atafutwe naibu waziri aliyelizungumzia.




Maoni ya wananchi


Albert Ryeyamamu, mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam, alisema utaratibu huo utawabana watumiaji wa simu ambao wakati mwingine wanamiliki laini zaidi ya moja kutokana na umuhimu wa matumizi kulingana na mitandao husika.


'Mfano mimi nina laini ya mawasiliano na nyingine naitumia kwa ajili ya intaneti, hiyo ni kutokana na unafuu wa gharama ninaoupata. Sasa unaponilazimisha niwe na namba moja itanipa wakati mgumu," alisema.


Naye Rehema Grey mkazi wa Kinondoni aliishauri Serikali kuangalia upya kabla ya kuanza utelekezaji wa mpango huo kwa kuwa unaweza kuharibu biashara kwa kampuni za simu na kuwabana watumiaji.


"Sioni kama ni sawa kwani huku ni kuingilia uhuru wa mawasiliano na athari yake haitakuwa kwa watumiaji tu, bali hata kampuni za simu zitakosa wateja kwa sababu watu tuna simu za laini mbili na matumizi yangu mfano hayawezi kufaa kwa namba moja pekee," alisema.




Kampuni zajipanga


Akizungumzia suala hilo, Mkuu wa Mawasiliano wa Halotel, Mhina Semwenda alisema hawajapata taarifa hiyo rasmi kwa kuwa yanapotokea mabadiliko kampuni za simu hupewa mwongozo. "Sisi wenyewe tumeona na kusikia kwenye mitandao, hatujapata taarifa rasmi kutoka kwa waziri mwenye mamlaka ya mawasiliano, hivyo siwezi kusema utaathiri au kuleta faida zipi," alisema.


Kwa upande wake, Ofisa Uhusiano wa Airtel, Jackson Mbando alisema taarifa hiyo wameipata kwenye vyombo vya habari na mitandaoni, lakini watakapoipata rasmi wataizungumzia.


Juhudi za kuwapata wasemaji wa kampuni zingine za mawasiliano hazikuzaa matunda.
Na Elizabeth Edward, Mwananchi
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...