Thursday, August 23, 2018

BOBI WINE ASHTAKIWA KWA KOSA LA UHAINI UGANDA

Mbunge wa Kyadondo nchini Uganda Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine ameshtakiwa kwa uhaini nchini.

Alikamatwa muda mfupi baada ya mahakama ya kijeshi kumuondolea mashtaka ya umiliki haramu wa silaha nchini.

Wine alikamatwa upya na kushtakiwa katika mahakama ya hakimu mkuu kujibu mashtaka ya uhaini pamoja na wabunge wengine waliokamatwa.

Mbunge huyo ambaye pia ni mwanamuziki nchini kwa jina maarufu Bobi Wine leo aliwasilishwa katika mahakama ya kijeshi mjini Gulu kaskazini mwa Uganda.

Mawakili wake awali walijuzwa kuwa kesi itasikilizwa katika kambi ya kijeshi ya Makindye anakozuiliwa mjini Kampala.

Kumekuwa na shinikizo kubwa kimataifa la kutaka Bobi Wine aachiwe huru.

Wengi nchini Uganda wanatazama kesi hii kama jitihada za kumnyamazisha mkosoaji mkuu wa serikali aliyechaguliwa kuwa mbunge mwaka jana tu.

Mawakili wa jeshi wameeleza mahakama kuwa mashtaka dhidi ya Wine yameondolewa na kwamba mwanasiasa huyo akabidhiwe kwa polisi ili akabiliwe na mashtaka ya uhaini pamoja na na wabunge wengine waliokamatwa.
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...