Saturday, August 25, 2018

Atiwa mbaroni kwa kosa la kuwaua wanawake 29 na kuwabaka

MKUU WA OPERESHENI MAALUM MAKAO MAKUU YA JESHI LA POLISI, NAIBU KAMISHNA WA POLISI (DCP), LIBERATUS SABAS.

JESHI la Polisi nchini, linamshikilia kijana mwenye umri wa miaka (27), mwenyeji wa Mkoa wa Mwanza kwa kosa la kubaka wanawake na watoto 28 baada ya kuwaua.

Mkuu wa Operesheni Maalum Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Liberatus Sabas, aliiambia Nipashe jana kuwa kijana huyo alikamatwa baada ya kukamatwa  watu 19 ambao walimtaja kuhusika na mauaji hayo.

Alisema polisi waliendesha operesheni maalum inayofanyika mikoa ya Mwanza, Shinyanga na Geita.

Sabas alisema kijana huyo ambaye jina lake limehifadhiwa kwa sasa kwa sababu za kiupelelezi, amekuwa akiwabaka wanawake na watu wenye umri kuanzia miaka 15 hadi 66 baada ya kuwaua.

"Mwezi Agosti mwaka jana matukio ya mauaji ya wanawake yalishamiri katika mikoa hii ya Shinyanga, Geita na Mwanza ndipo mwezi huu kuanzia tarehe 8 tulipoanza operesheni hii ya kusaka wanaofanya mauaji haya," alisema.

Mkuu huyo alisema katika mkoa wa Mwanza matukio hayo yalishamiri wilaya ya Misungwi ambako wanawake waliokuwa wakienda kwenye shughuli za kujitafutia riziki, walikuwa wakiuawa.

"Katika operesheni hii tulikamata watu 19 na saba kati yao tumewaachia baada ya uchunguzi. Waliobaki ni 12 ambao tumewakuta na vielelezo mbalimbali zikiwamo simu nne ambazo ni za wanawake waliouawa," alisema.

Alisema baada ya kutajwa na wenzake, kijana huyo alikamatwa na alipohojiwa alikiri kuwaua wanawake na watoto 29 na kwamba baada ya mauaji hayo alikuwa akiwaingilia kimwili.

"Kati ya watu 29 aliowataja kuwafanyia mauaji hayo, mmoja alinusurika kifo baada ya kumpiga mawe na kudhani amemuua na kumbaka. Mwanamke huyo aliokotwa na kupelekwa hospitalini ambako alikaa kwa muda wa siku tano bila kujitambua kutokana na hali yake kuwa mbaya," alisema.

Kwa mujibu wa Sabas, kijana huyo aliwaeleza kuwa amekuwa akifanya matukio hayo kutokana na imani za kishirikina kuwa atapata utajiri.

"Huyu kijana ni mzima hana matatizo ya akili na anajieleza vizuri namna alivyokuwa akitekeleza mauaji hayo na kisha kuwabaka wanawake na watoto, ametueleza kuwa alikuwa na uwezo wa kuwabaka wanawake wanne aliowaua kwa siku," alisema.

Alisema kijana huyo amewaeleza kuwa alikuwa akifanya vitendo hivyo kwa namna tofauti kwani kama wanawake watakuwa zaidi ya mmoja, amekuwa akiwatishia na wakati wakikimbia anamkamata mmoja ndipo anamuua na kumbaka.

"Huyu kijana ni wa ajabu kwa kweli hana huruma. Anasema akimkamata mwanamke au mtoto anamnyonga au anampiga mawe hadi afe ndipo anambaka," alisema.

Kwa mujibu wa Sabas, kijana huyo aliwaambia kuwa moja ya matukio aliyofanya ni alipokutana na wanawake wakiwa wamebeba mapanga lakini aliwazidi nguvu na kuwapiga mawe na baada ya wengine kukimbia na yeye  kumkamata mmoja, alimuua kwa mawe na kumbaka.

Kuhusu operesheni hiyo, Kamanda Sabas alisema ni endelevu na lengo lake ni kuokoa maisha ya wanawake ambao ilifikia mahali walikuwa wakishindwa kutoka nyumbani kwenda kufanya shughuli zao za kila siku.

"Mwanamke alikuwa akienda kuchota maji, kuokota kuni, akienda gulioni, au popote alikuwa akikutana na kijana huyu anauawa, tumedhamiria kuvikomesha vitendo hivi na yapo mambo mengi ambayo tumeyapata ambayo kwa sababu za kiintelijensia hatuwezi kuziweka hadharani,"alisema.

"Itoshe kuwaeleza wanawake wa mikoa hii kuwa operesheni hii ina lengo la kurudisha amani kwao kwa sababu wengi wao walifikia hatua ya kushindwa kufanya shughuli zao," aliongeza.

Alisema katika operesheni hiyo wamebaini kuwa wilaya za Kwimba, Misungwi mkoani Mwanza na Shinyanga  ndizo zimeathirika zaidi na matukio hayo.
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...