Monday, May 5, 2025

Gambo Amjibu Paul Makonda 'Arusha Hatutapeliki....'




Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo, ameibuka hadharani na kupinga vikali madai ya baadhi ya viongozi wanaodai kuwa fedha za ujenzi wa barabara ya Eso–Longdong jijini Arusha zilitolewa na Serikali Kuu, akisema fedha hizo zilitengwa kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Arusha.

Akizungumza mwishoni mwa wiki jana mbele ya wananchi wa Kata ya Sokoni 1, Gambo ameonesha kukerwa na madai hayo na kuyataja kuwa ni ya kitapeli, akiwataka viongozi waache kutafuta sifa kwa kazi ambazo hawajahusika nazo.


"Mwaka jana tulitenga fedha kwa ajili ya barabara hii, lakini zikaelekezwa kwingine. Mwaka huu tumerudia tena, tumetenga milioni 900 kupitia mapato ya ndani ya jiji letu. Hakuna fedha kutoka Serikali Kuu," amesema Gambo.

Ameongeza kuwa wananchi wa Arusha wanahitaji vitendo, si porojo, akisisitiza kuwa hawadanganyiki na hawatapeliwi kirahisi.

"Nilisikia mtu anasema eti ameleta fedha. Mwambieni aache utapeli. Arusha hatudanganyiki na hatutapeliki!" ameongeza kwa msisitizo.


Kauli ya Gambo imeibuka wakati mvutano wa kisiasa ukiendelea baina yake na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, huku pande zote zikirushiana maneno kuhusu uhalali wa mafanikio ya miradi ya maendeleo jijini humo.


Hivi Karibuni Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda amemtaka Mbunge wa jimbo la Arusha mjini Mrisho Gambo kuwaomba msamaha hadharani watu wote aliowahi kuwaumiza,kuwachonganisha nakuharibu maisha yao

Makonda alitoa kauli hiyo mbele ya Naibu waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt Doto Biteko kwenye maadhimisho ya miaka 61 ya uhuru wa Tanganyika na Zanzibar ambayo yamefanyika katika viwanja vya Kilombero Mkoani Arusha


"Nampongeza kwasababu moja kubwa, juzi ameomba radhi Bungeni, amechonganisha chonganisha sana Watu hapa na leo hapa ameanza kumsifia Mkuu wangu wa Wilaya kwa sifa zilezile ambazo alinisifiaga Mimi nilipoteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa lakini sasa hivi hata kulitamka jina la Makonda hawezi"

"Namsifu kwa sababu aliomba radhi, alikuwa anaenda kuharibu maisha ya Watu kwa kuwadanganya Wabunge na kama Bunge lisingekuwa makini na Waziri wetu Mchengerwa kuwa imara, leo hii kuna Watu wangepoteza kazi kwasababu yake"


"Sasa ombi langu kwake moja awaombe radhi Watu wote aliowafitini kwa kuwaumiza, kuwachonganisha na kuharibu maisha yao, safari ya Mbinguni hata Mimi naitaka, mambo yalivyoendelea yalipelekea simu ninazopata, unamuita Waziri wetu muongo?, hii stendi inayoanza kujengwa, hii nimemuomba Mchengerwa, ilikuwa design ndogo haikidhi viwango, akaongeza bajeti bilioni 30 ni faida kwa Wanancgi wa jiji, halafu unamuita Waziri wetu muongo!?"


"Kwa kuwa Bunge limemsamehe, Mimi moyoni sina shaka nae lakini sharti langu moja aliowaumiza na kuharibu maisha yao awaombe radhi ili mbele ya Mungu na mbele ya Wanadamu tupate kibali cha kuifanya kazi hii"


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...