Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Dominic Raab, amesema nchi hiyo itatoa hifadhi kwa wafanyakazi wa vyombo vya habari vya Afghanistan waliofanya kazi na mashirika ya Uingereza, na ambao sasa wanakabiliwa na vitisho kutoka kwa kundi la Taliban.
Akijibu katika gazeti la Uingereza la The Times barua ya wazi iliyoandikwa na magazeti makuu ya nchi hiyo yaliyotoa wito kwa serikali kuwapa hifadhi raia hao wa Afghanistan, Raab amesema mpango wa kuwapa hifadhi utazingatia watu wenye kesi maalum.
Magazeti ya Uingereza pamoja na vituo vya televisheni vya Sky News na ITN, yalitia saini barua walioiwasilisha kwa serikali, na kuonya kuwa mashambulizi ya Taliban yaliyochochewa na kuondoka na vikosi vya kimataifa vya usalama kunawaweka katika hatari waandishi wa habari wa Afghanistan.
Kundi la Taliban sasa linadhibiti sehemu kubwa ya Afghanistan na limekuwa likizidisha mapambano dhidi ya vikosi vya serikali katika miji mikuu ikiwemo Herat, karibu na mpaka wa magharibi na Iran na mji wa upande wa kusini wa Kandahar.