Benki ya NMB imeshinda tuzo mbili za kimataifa 'kwa mpigo,' za Benki Bora Tanzania na Benki Bora ya Huduma kwa Wateja Binafsi na Biashara za Kati, Tanzania, zilizotolewa na majarida maarufu yanayoangazia huduma za kifedha duniani.
Jarida la Euromoney limeitangaza NMB kuwa mshindi wa Tuzo ya Benki Bora Tanzania kwa mwaka wa tisa mfululizo, huku Global Banking and Finance, likiitaja kama Benki Bora ya Huduma kwa Wateja Binafsi na Biashara za Kati nchini.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi tuzo hizo kwa Bodi ya Wakurugenzi wa NMB, Afisa Mtendaji Mkuu wa benki hiyo, Ruth Zaipuna, alisema NMB inajivunia ufanisi uliozaa tuzo hizo, huku akitaja siri za mafanikio hayo.
Akimkabidhi tuzo hizo Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa NMB, George Mulamula, Zaipuna alisema ubunifu wa bidhaa, uwekezaji kiteknolojia na suluhu za kidigitali ni kati ya mambo yaliyochangia kuifanya NMB kuwa benki bora.
Zaipuna aliongeza kuwa, tuzo hizo kutoka Euromoney na Global Banking and Finance, majarida yenye Makao Makuu London, Uingereza, ni kielelezo kuwa juhudi za benki zinatambuliwa si tu Tanzania, bali hata na taasisi za kimataifa..
"Ni heshima na mafanikio makubwa kwa NMB kupata tuzo hizi. Tunajivunia kuona juhudi zetu zinatambuliwa kimataifa na tunajiona tuna deni la kuendelea kujituma zaidi ili kubaki kwenye viwango vya kimataifa kama benki bora," alisema.
Akipokea tuzo hizo, Mulamula aliyemwakilisha Mwenyekiti wa Bodi, Dk. Edwin Mhede, alisema tuzo hizo zina maana kubwa kwao, huku akiupongeza uongozi wa benki hiyo na wafanyakazi kwa mafanikio hayo na kuwataka kutobweteka.
"Naipongeza Menejimenti na wafanyakazi kwa utendaji wao mzuri uliosababisha ushindi huu. Tuzo ya Euromoney ni ya mwaka wa tisa mfululizo na pia Global Banking and Finance kuitambua NMB kama Benki Bora ya Huduma kwa Wateja Binafsi na Biashara za Kati.
"Ningependa ieleweke kwa jamii na wateja wetu kuwa, tuzo hizi zina maana moja kubwa kwamba NMB ni benki bora hapa Tanzania na tumejikita katika kutoa huduma bora kwa Watanzania magali popote walipo mijijini na vijijini.
"Nawashukuru wateja na Watanzania kwa kuifikisha NMB hapa, wajibu wetu ni kuendelea kuwa benki bora inayoakisi kasi ya Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan. Uongozi na wafanyazi wasibweteke, waongeze ufanisi ili kubaki juu kwa ubora," alisema Zaipuna.
Tuzo hizo zimetolewa kwa kuzingatia vigezo kadhaa kwa benki zilizopendekezwa, ukiwamo ufanisi wa mahesabu na utendaji kwa ujumla, mkakati wa huduma za kidijitali, huduma jumuishi za fedha, usalama wa huduma za kimtandao na uwajibikaji wa benki katika jamii inayoizunguka.
Vigezo vingine vilivyotumika ni mtaji wa benki, mapato yatokanayo na mali za kampuni, pato litokanalo na riba, uwiano wa fedha na gharama za uendeshaji, kiwango cha amana za wateja na kiwango cha mikopo katika soko.
Pia limo vigezo vya uwiano kati ya mikopo na amana za wateja, uwiano wa mikopo chechefu, na uwiano wa hasara itokanayo na mikopo chechefu.