Sunday, July 18, 2021

VIJANA WA CCM SHINYANGA WAMUOMBA RAIS SAMIA KUTAZAMA UPYA SUALA LA TOZO YA MIAMALA YA SIMU...'LINAUMIZA'


Mwenyekiti wa UVCCM, Baraka Shemahonge akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Vijana wa CCM mkoa wa Shinyanga.

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Baraza la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Shinyanga likiongozwa na Mwenyekiti wa UVCCM, Baraka Shemahonge wamemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kulitazama kwa taswira mpya suala zima la tozo za miamala ya simu kwa manufaa ya wananchi wa hali ya chini na Ajira za vijana wengi wanaojipatia kipato kutokana na shughuli za kutuma miamala kwani mzunguko miamala ya simu za mkononi utapungua.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa UVCCM, Baraka Shemahonge Julai16,2021 katika kikao cha Baraza la Vijana wa CCM mkoa wa Shinyanga ambacho kimehudhuriwa na mkuu wa mkoa huo Dkt. Philemon Sengati aliyekuwa mgeni rasmi katika kikao hicho pamoja na Naibu Waziri wa Vijana Kazi na Ajira, Patrobas Katambi ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini na Mbunge wa Kundi la Vijana Mwasi Kamani.

"Baraza la Vijana linampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya tangu kuingia kwake madarakani ikiwemo kukuza maendeleo pamoja na kuendeleza miradi mikubwa ya kimkakati nchini .Tangu kuingia kwake madarakani upo mwanga na matumaini kwa wananchi. Tunamuomba Mhe. Rais kulitazama kwa taswira mpya suala zima la tozo za miamala ya simu ambalo limezua gumzo kila mahali",amesema Shemahonge.

Shemahonge amesema wanamuomba Mhe. Rais Samia alitazame upya jambo la Tozo za miamala ya Simu akibainisha kuwa wana imani kila Mtanzania yuko tayari kuchangia maendeleo ya nchi yake kwani Tanzania itajengwa na Watanzania wenyewe lakini tozo imekuwa kubwa kidogo.

"Tunaona vijana wengi watakosa ajira kwa sababu mzunguko wa miamala ya simu utapungua lakini wazee na wananchi waliopo vijijini wataathirika kwa sababu kule hakuna Benki, wengi wao wanatumia Simu kutuma na kutumiwa fedha. Kwa makato haya yanakwenda kuathiri moja kwa moja wananchi wenye kipato chaa chini",amesema Shemahonge.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Philemoni Sengati amewaomba vijana wa UVCCM Mkoa kuendelea kuhamasisha Falsafa ya kujitegemea kiuchumi kwa vijana na kuwa wabunifu wa fursa mbalimbali huku akiafiki ombi la ujenzi wa Chuo Kikuu ambacho kitakuwa kichocheo cha uchumi wa mkoa wa Shinyanga.

Dkt. Sengati pia amechangia Shilingi milioni 2.5 kwa ajiri ya ujenzi wa nyumba ya Katibu wa Vijana wa CCM mkoa wa Shinyanga.
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...