Sunday, July 4, 2021

Takribani watu 17 wapoteza maisha katika ajali ya ndege, wengi waokolewa

Takribani watu 17 wamepoteza maisha katika ajali ya ndege ya jeshi kusini mwa Ufilipino, lakini watu 40 wameokolewa wakiwa hai kutoka kwenye mabaki ya ndege iliyoteketea kwa moto.

Ndege hiyo ya kijeshi ilikuwa imebeba watu 92, wengi wao vikosi vya kijeshi, wakati ilipozidi barabara yake kuu ya kisiwa cha Jolo.

Walionusurika walipelekwa kwenye hospitali ya kijeshi iliyo karibu. Miili 17 ilipatikana kwenye eneo la ajali.


Moshi mwingi mweusi ulionekana juu ya mabaki ya ndege, aina ya Lockheed C130 Hercules.

Shirika la habari la serikali lilionesha picha za tukio hilo, mabaki yaliyokuwa yakiungua katika eneo lililo karibu na majengo kadhaa.

Ndege hiyo ilianguka majira ya saa tano na nusu kwa majira ya eneo hilo, kilomita chache kutoka mji wa Jola, ndege ilibeba wanajeshi kutoka mji wa Cagayan de Oro, katika kisiwa cha kusini cha Mindanao.

''Ilikosea njia yake, ilipokuwa inajaribu kurejea katika njia sawia haikufanikiwa,'' Mkuu wa jeshi Jenerali Sobejana aliwaambia waandishi wa habari.

Wanajeshi hao walikuwa sehemu ya wanajeshi wa nyongeza huko kusini mwa Ufilipino ili kupambana na wanamgambo wa Kiislam kama vile kundi la Abu Sayyaf.

Maafisa walisema hakukuwa na ishara kwamba ndege hiyo ilishambuliwa, na uchunguzi utaanza mara tu shughuli ya uokoaji itakapokamilika.

Wengi wa wale waliokuwamo kwenye ndege hiyo walikuwa wamemaliza mafunzo ya msingi ya kijeshi, AFP imeripoti.

Ndege hiyo, iliyokuwa ikihudumu na Jeshi la Anga la Marekani, ilikabidhiwa Ufilipino mwezi Januari. Ilikuwa ya kwanza kati ya ndege mbili aina ya Hercules zilizotolewa na Marekani chini ya mpango wa ushirikiano wa ulinzi.

Ndege hiyo iliruka kwa mara ya kwanza mnamo 1988, kulingana na Mtandao wa Usalama wa Anga.

 

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...