Friday, July 9, 2021

RC Pwani awataka viongozi wa dini kukemea uhalifu

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Aboubakar Kunenge, ametoa onyo kali kwa watu wanaoendelea kujihusisha na uhalifu mbalimbali licha ya serikali kutoa matamko mbalimbali kuwa hatua stahiki za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

RC Kunenge ametoa onyo hilo wakati akizungumza na viongozi wa madhehebu mbalimbali mkoani Pwani, amesema wameshatoa matamko mengi lakini wapo baadhi ya watu bado wanaendelea kujihusisha matukio hayo ambayo ni kero kwa wananchi.

"Tumetoa matamko mengi ya kuwataka watu waache kujihusisha na uhalifu lakini baadhi bado wanaendeleza vitendo hivyo lakini kwa sasa tumefika mwisho, Serikali imekuwa ikijitahidi kutoa elimu na ushauri kwa wananchi kutojihusisha na vitendo vya uhalifu lakini bado wanaendeleza vitendo vya kihalifu," alisema RC Kunenge.

Pia RC Kunenge amewaasa viongozi wa dini kushirikiana na serikali kuwatangazia waumini wao juu ya kuacha vitendo hivyo viovu ikiwemo wizi, ubakaji, kuvamia nyumba za ibada na matumizi ya dawa ya kulevya na uingizwaji wa wahamiaji haramu.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...