Dar es Salaam. Ni mnyukano wa hoja dhidi ya hoja kati ya Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro na Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu.
Wakati Sirro akidai kuwa Lissu alikaidi wito wa jeshi hilo kuhojiwa kuhusu tukio la kushambuliwa kwake, kiongozi huyo wa upinzani amekanusha madai hayo akisema hajawahi kuitwa kwa suala hilo.
Akizungumza juzi katika kipindi cha Medani za Siasa kinachorushwa na kituo cha runinga cha Star TV, IGP Sirro alidai kuwa alimpigia simu Lissu wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka 2020 akimtaka afike polisi kuhojiwa kuhusu tukio hilo lakini hakufika.
Septemba 7, 2017 Lissu alishambuliwa kwa risasi 16 akiwa anahudhuria vikao vya Bunge jijini Dodoma na baadaye alikwenda kutibiwa Nairobi Kenya kabla ya kuhamishiwa Ubelgiji tangu Machi 2018, anakoishi mpaka sasa.
Lakini Sirro alisema katika mahojiano hayo kuwa Lissu hataki ushirikiano na vyombo vya dola.
"Tundu Lissu hataki ushirikiano na vyombo vya ulinzi na usalama. Polisi tumemwita mara nyingi, mimi nimeshampigia simu. Nilishampigia Tundu Lissu simu wakati amekuja kwenye kampeni zake kwamba, njoo tukuhoji utujulishe kilichotokea. Nikamwambia tuonane tuzungumzie hiki kilichotokea, akakaidi. Huyu bwana by nature (kwa asili) ni mkaidi," alisema Sirro.
Hata hivyo, madai hayo yamepingwa na Lissu katika maneno yake aliyoyaweka katika ukurasa wake wa Twitter akisema ni uongo.
"IGP Sirro hajawahi kunipigia simu au kuniita kwenye mahojiano yoyote. Nikiwa Nairobi Hospital niliambiwa polisi watakuja kunihoji hospitalini. Niliwasubiri lakini hawakuonekana.
"Polisi hawajahoji mtu yeyote wala kutoa taarifa yoyote juu ya uchunguzi wao, zaidi ya kudai wahusika ni watu wasiojulikana na hakuna hata mtu wanayemshuku," aliandika Lissu.
Kama hiyo haitoshi Lissu alisema wakati wa kampeni za uchaguzi alikwenda polisi Dodoma kudai gari lake ambalo liko polisi tangu aliposhambuliwa, lakini alikataliwa kulichukua.
"Jibu lilikuwa sitapewa gari yangu mpaka nitakapohojiwa juu ya shambulio. Lakini polisi hawakuwa na mpango ya kunihoji zaidi ya kupiga mabomu mikutano yangu ya hadhara," alisema Lissu.
Alisema baada ya shambulio hilo, Jeshi la Polisi lilizuia jitihada za waliotaka kumpa msaada.
"Waliojaribu kuniombea kanisani na msikitini walipigwa marufuku. Waliojaribu kujitolea damu walikatazwa. Waliovaa T-shirt (fulana) zenye picha yangu walikamatwa na kuwekwa mahabusu," alisema.
Waliomshambulia Lissu
Kwa upande mwingine, IGP Sirro aliulizwa pia sababu ya kutojulikana kwa waliomshambulia Lissu mpaka sasa, alisema kiongozi huyo wa Chadema ni binadamu kama wengine hivyo anaweza kuwa na maadui.
"Kwa nini tuzungumzie Lissu, tuzungumzie Watanzania wote wanaopata madhara kwa sababu Lissu hana tofauti na binadamu wote wanaopata madhara," alisema.
Katika maelezo yake, Lissu alisema kuwa polisi walikuwa na picha za kamera za CCTV iliyokuwa kwenye jengo aliloshambuliwa. "Hadi leo wako kimya juu ya hilo. Polisi hawajawahi kusema ni nani aliyeondoa walinzi wote kwenye makazi ya viongozi wa Serikali ili kuwaruhusu wauaji waingie ndani na kunishambulia kwa risasi," alidai.
Alipoulizwa kuhusu madai ya Lissu kutoa taarifa za kufuatiliwa na magari asiyoyaelewa siku chache kabla ya kushambuliwa kwake, IGP Sirro alikanusha akisema hakukuwa na taarifa hizo katika jeshi lake kuhusu Lissu kutishiwa.
"Jeshi langu halijawahi kuwa na taarifa yoyote kuhusiana na kutishiwa kwa Lissu. Na nilishangaa kusikia anasema amekuwa akiripoti polisi mara kwa mara," alisema IGP Sirro.
"Ukiripoti kituo cha polisi unaacha rekodi pale, wataandika maelekezo yako watafanya nini, na wewe kwa sababu ni mwanasiasa utakwenda kumwona OCD, RPC, atakwambie alikwenda kumwona nani."
Kuhusu kuhakikishiwa usalama wake, Sirro alisema Lissu hawezi kupewa ulinzi peke yake bali atachukuliwa kama Mtanzania wa kawaida.
"Ana maana gani kuhakikishiwa usalama wake? Suala zima, Watanzania wote wako salama. Watanzania wote wapo salama wanafanya maendeleo yao, wanazaa watoto wao wanapata maendeleo yao wanaishi Tanzania sasa wewe ni Mtanzania mmoja unahakikishiwa kivipi wakati Watanzania wengi wana amani wanafanya shughuli zao?" alihoji Sirro
"Hatuwezi kutoa ulinzi kwa kila mtu, yeye arudi hapa nchini aone kama atapata tatizo na akipata tatizo aripoti Polisi kama Mtanzania mwingine,'' aliongeza.
Akijibu hoja hiyo, Lissu aliandika kwenye Twitter: "IGP Sirro anasema sistahili kupewa ulinzi wowote kwa sababu mimi ni Mtanzania sawa na Watanzania wengine. Lakini sio Watanzania wote waliowahi kushambuliwa kwa risasi 16 wala kutendewa kama nilivyotendewa mimi."
Mwananchi