Monday, July 12, 2021

Mawaziri wakutana kujadiri suala la mgao wa mrabaha kwa kazi za wasanii

 


Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Dkt .Faustine Ndugulile MB, pamoja na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa wamekutana katika kikao cha pamoja kujadili namna Wizara wanazozisimamia zitakavyotekeleza suala la mgao wa mrabaha kwa kazi za wasanii wa muziki zinazochezwa kwenye vyombo mbalimbali vya Habari.

Katika kikao hicho kilichofanyika jijini Dar es Salaam, Mawaziri hao wawili wamekutana na Wakurugenzi wakuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Chama cha Hatimiliki Tanzania (COSOTA), Makatibu Wakuu wa Wizara zote mbili pamoja na wataalaam kutoka Kituo cha data cha Taifa,TCRA na wizara.

Kikao kazi hicho kimejadili na kuweka mikakati ya pamoja juu ya utekelezaji wa zoezi la kuanza rasmi kwa mgao wa mrabaha kwa wasanii, pia wamejadili na kupitia mapendekezo ya marejeo ya Kanuni za Maudhui Mtandaoni ili kuona uwezekano wa kupunguza au kufuta baadhi ya tozo za leseni za maudhui mtandaoni.

Wamekubaliana kuhakikisha miundombinu itakayowezesha ukusanyaji wa mirabaha inawekwa katika hali ya utayari huku Mawaziri wakiziagiza taasisi za TCRA, Kituo cha Data na COSOTA kuhakikisha mifumo husika itakayohusika kukokotoa mirabaha inakamilika na kufanya kazi kwa wakati kama ilivyokusudiwa.

Katika kikao hicho Mawaziri walipokea na kujadili taarifa za maandalizi ya ufuatiliaji maudhui na namna maudhui ya kazi za muziki za wasanii zitakavyokokotolewa ili kuhakikisha wasanii wa muziki wanapata haki yao ya mapato yatokanayo na kazi zao za sanaa ya muziki.


Pia walijadili mapendekezo ya marekebisho ya kanuni za utangazaji na mfumo wa leseni unaopendekeza maboresho katika mfumo wa upatikanaji wa maudhui ya bila kulipia na ya kulipia, kanuni zinazotarajiwa kuanza kutumika hivi karibuni baada ya taratibu bayana kukamilika.


Awali Mkuu wa COSOTA akitoa taarifa mbele ya waheshimiwa Mawaziri alibainisha kuwa mara zoezi la ulipaji mirabaha litakapoanza watahakikisha kila aliechangia kufanikisha kazi ya msanii husika kukamilika hadi kurushwa anapokea stahiki yake, aliwataja baadhi ya wahusika hao kuwa ni pamoja na watayarishaji wa muziki, waandishi wa mashairi na lebo za muziki.


Source
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...