Mahakama ya juu ya rufaa nchini Misri leo imeunga mkono hukumu ya kifungo cha maisha gerezani dhidi ya viongozi kumi wa kundi lililopigwa marufuku nchini humo la Udugu wa kiislamu akiwemo kiongozi wa kundi hilo Guide Mohamed Badie.
Haya yameripotiwa na shirika la habari linaloendeshwa na serikali la MENA.Mnamo mwaka 2019, mahakama ya uhalifu ya Cairo iliwatia hatiani watu hao kwa makosa yanayohusiana na mauaji ya polisi na njama ya kutoroka kwa wafungwa wengi wakati wa maandamano makubwa ya mwaka 2011 nchini humo.
Washtakiwa hao walipatikana na hatia ya kuwasaidia wafungwa elfu 20 kutoroka na pia kuhujumu usalama wa taifa kwa kushirikiana na makundi ya wanamgambo wa kigeni ya Hamas katika mamlaka ya Palestina na Hezbollah nchini Lebanon.
Wakati huo huo, mahakama hiyo ya rufaa imewaondolea mashitaka viongozi wanane wa cheo cha kati wa kundi hilo kongwe zaidi la msimamo mkali wa kidini ambao awali walikuwa wamehukumiwa kifungo cha miaka 15 gerezani.