Dk. Anthony Diallo, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mwanza
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Mwanza, Dk. Anthony Diallo ameomba radhi 'kiaina' baada ya kauli yake kuzua mjadala ndani na nje ya chama chake. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mwanza … (endelea).
Dk. Diallo amesema, ametafasiriwa vibaya na baadhi ya watu huku akiwataka wanachama wa chama hicho tawala nchini Tanzania kuwa makini kwani wapo wasiowatakia mema wanatumia mwanya huo kuwachonganisha.
Ni baada ya jana Jumamosi, tarehe 10 Julai 2021, kuzungumza masuala mbalimbali yaliyojitokeza katika utawala wa awamu ya tano akigusia suala la nchi kuongozwa kwa matamko.
Dk. Diallo aliyewahi kuwa waziri, alizungumza hayo katika kipindi cha Ajenda, kinachorushwa na kituo chake cha televisheni cha Star TV, jijini Mwanza.
Akijibu swali la mwandishi wa habari aliyetaka kupata maoni yake juu ya nchi kuongozwa kwa matamko bila kufuata Katiba na sheria, Dk. Diallo alisema, kuna umuhimu wa kuangalia historia ya mtu kabla ya kupewa dhamana ya kuongoza.
"Mimi nafikiri tuwe waangalifu tu katika kuchagua tuwe tuna 'track record' kwani huko nyuma tuliwahi kuchagua watu walikwisha kwenda hospitali za vichaa 'milembe' harafu unamwachia aongoze nchi, kwa hiyo tuwe makini," alisema.
Kauli hiyo ilizua mjadala na leo Jumapili, tarehe 11 Julai 2021, akizungumza na waandishi wa habari amesema "nilifanya kosa kwa kutolea mfano wa wakati uliopita badala ya wakati ujao kuwa tusipokuwa waangalifu tunaweza kuchagua viongozi wenye matatizo ya akili."
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM), Kenani Kihongosi
"Na sijasema mtu kuwa aliyekuwa na tatizo ila nilikosea tu kwenye maelezo. Nawataka radhi wale ambao walinielewa vibaya kwani wapo waliotafasiri wanavyojua wao," amesema Dk. Diallo.
Mwanasiasa huyo mkongwe nchini amsema "mimi nadhani tuwe waangalifu sana hasa wana CCM, tumeanza kuingiliwa sana."
Dk. Diallo amekosoa kitendo cha baadhi ya viongozi wa chama hicho kuanza kutoa matamko kabla ya kumsikiliza au kumuuliza alikuwa ana maanisha nini.
"Unakuta ni kiongozi wa chama anatoa tamko na kunituhumu kama vile nimefanya kosa, bila hata kuniuliza. Lazima tuwe waangalifu sana wana CCM," amesema Dk. Diallo.
Soma zaidi:-
Miongoni mwa viongozi waliomshtumu ni Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM), Kenani Kihongosi alisema, viongozi walioaminiwa na "chama chetu, na wanakaa katika vikao vya maamuzi, tunawaomba wawe na nidhamu na chama hiki."
"Chama hiki ni kikubwa kuliko mtu, kwa hiyo mwenyekiti na katibu mkuu wetu, niwaombe sisi kama UVCCM, kauli ile imetuudhi sana, mwenyekiti wa CCM anapozungumza hivyo hapaswi kuungwa mkono."
Kihongosi aliongeza kwa kusema "kama yeye aliona wanapaswa kwenda milembe hapa anafanya nini, kama ni vikao vya maamuzi yeye ni miongoni na kauli zile kama sisi vijana zinatuvunja moyo."