NAIBU Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi, amesema mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira (DAWASA) imepiga hatua kubwa katika usimamizi wa miradi ya maji nchini, ikiwemo matumizi mazuri ya fedha na kuwezesha kuwekeza Sh Bilioni 17.8 katika mradi wa maji ukiwemo wa Ruvu Juu mpaka Msoga.
Mradi huo utakapokamilika unatatua kero ya maji kwa wananchi zaidi ya 122,000 wa maeneo hayo.
Alisema Dawasa chini ya Afirsa Mtendaji Mkuu, Cyprian Luhemeja imefanikiwa
kutekeleza miradi takribani 27 sehemu mbalimbali ya Dar es Salaam na Pwani.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Miundombinu na Uwekezaji DAWASA, Mhandisi Ramadhani Mketo, amesema mradi wa maji wa Ruvu Juu hadi Mboga ni mradi utakaosaidia kuondoa kero ya maji katika maeneo ya Mlandizi, Chalinze na Mji Mdogo wa Mboga.
Pia Mradi huo kwa sasa wanalaza mabomba kwa umbali wa Kilometa 59 katika Mitambo ya Ruvu Juu hadi Chalinze, Mji wa Mboga.
Aidha amesema mradi huo ukikamilika utatua kero ya Maji katika Bandari Kavu ya Kwara na kwenye Mradi wa Reli ya Kisasa ya SGR Kwara, amesema lita 9,300,000 za Maji zitatumika kwa siku baada ya kukamilika mradi huo.
Naye, Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Ridhwan Kikwete, amesema ujio wa Naibu Waziri wa Maji, katika maeneo hayo utasidia katika utekelezaji wa miradi hiyo ya Maji na kuondoa kero kwa wananchi wake.