Na John Walter-Babati
Wananchi wa wilaya Babati Mkoani Manyara wamefurahishwa na kasi ya utekelezaji wa baadhi ya ahadi za mbunge wao Daniel Sillo alizozitoa wakati wa kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu 2020 hali iliyoanza kuwajengea matumaini makubwa kwa serikali awamu ya sita.
Wakitoa maoni yao kwa nyakati tofauti wakati wa ziara ya mbunge wa jimbo la Babati vijijini Mhe. Daniel Sillo alipozitembelea kata za Nkaiti na Mwada wananchi hao wamesema kuwa kitendo cha kuwatembelea na kusikiliza kero zao na kuzijibu kinawatia moyo na kuona uwakilishi wake bungeni.
Wamesema kuwa kitendo cha mbunge huyo kurejea jimboni na kuanza kutekeleza ahadi alizozitoa kwa wananchi tena kwa kipindi kifupi kimewagusa sana na kuanza kuamini kuwa changamoto sugu zilizowasibu kwa kipindi kirefu sasa ikiwemo maji na bara bara zitaanza kutatuliwa na kuwafanya kuishi bila malalamiko.
Mh. Sillo ameanza ziara maalum ya Kata hadi Kata katika Vijiji vya Jimbo hilo ili kutatua, kushukuru, kusikiliza kero baada ya hivi karibuni kuhitimisha Bunge la Bajeti.
Amesema baada ya kuhitimisha bunge la bajeti 30 Juni mwaka huu, ameona ni wakati sasa wa kurejea tena kwa Wananchi.
Aidha, Mhe. Sillo amekuwa mstari wa mbele katika kutanguliza maslahi ya umma haswa wananchi wake amekuwa akiwasilisha kero mbalimbali Bungeni katika kutatua ambapo pia ameshashughulikia kero za maji safi na salama, Umeme, Miundombinu na mengine mengi ikiwemo kushirikiana na wananchi wa jimbo katika shughuli za kijamii kwa kutoa misaada mbalimbali katika shule za msingi na sekondari.
Katika ziara hiyo iliyofanywa kwenye Kata za Mwada na Nkaiti, Sillo alifanya mikuatano kwa kukutana na wananchi wa vijiji hivyo kwa kuwaeleza juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali Mafanikio na changamoto zilizopo pamoja na kusikiliza kero,maoni na ushauri kutoka kwa wananchi hao.
Mheshimiwa Daniel Sillo amewaeleza wananchi juu ya adhma ya Serikali kuwatumikia wananchi kwa kuwaletea maendeleo ili wananchi wanufaike kutokana na kodi zinazokusanywa na serikali kwa kujenga miundo mbinu na kuwaletea wananchi huduma mbalimbali.
"Wananchi wa Babati mmenipa dhamana ya kuwatumikia lakini chini ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano Wa Tanzania mama yetu Samia Suluhu Hassan, mimi ninawambia sitawaangusha." amesema Mheshimiwa Sillo.
Aidha Mheshimiwa Sillo amewataka wananchi kuendelea kuiamini serikali na kutoa ushirikiano ili kuweza kutatua changamoto zinazowakabili kwenye maeneo yao kwa urahisi.
Mbunge Sillo pia aliambatana na ujumbe kamili wa Chama Cha Mapinduzi wakiongozwa na Katibu wa Chama Wilaya Ndugu Filbert Mdaki,viongozi wa serikali kwa upande wa Tarura na Afya.