Aliyekuwa askari polisi, mwenye namba F 6763 Koplo Deodatus Massare (37) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na shtaka moja la kusafirisha dawa za kulevya aina Heroine, zenye uzito wa kilo 1.04.
Massare, ambaye ni mkazi wa Bunju Moga, wilaya ya Kinondoni, amefikishwa Mahakamani hapo leo Alhamisi, Julai 15, 2021 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 57/2021.
Mshtakiwa huyo amesomewa shtaka lake na wakili wa Serikali, Sylvia Mitanto mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Joseph Luambano.
Awali, kabla ya kusomewa shtaka hilo, hakimu Luambano amesema mshtakiwa hatakiwi kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi za uhujumu uchumi isipokuwa kwa kibali maalumu.
Akimsomea hati ya mashtaka, wakili Mitanto, amedai kuwa mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa lake, Juni 19, 2021 eneo Bunju Beach wilaya ya Kinondoni.
Siku hiyo ya tukio, mshtakiwa anadaiwa kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroine zenye e uzito wa kilo moja 1.04kg kinyume cha sheria.
Mshtakiwa baada ya kusomewa shtaka lake, upande wa mashtaka umedai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na hivyo kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hakimu Luambano baada ya kusikiliza maelezo hayo, ameahirisha kesi hiyo hadi Julai 29, 2021 itakapotajwa.
Mshtakiwa alirudishwa rumande kwa sababu kesi inayowakabili haina dhamana kwa mujibu wa sheria.