Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis leo hii amehimiza kutolewa msaada wa kiutu kuwafikia watu wanaokabiliwa na njaa katika eneo la vita la jimbo la Tigray, kaskazini mwa Ethiopia.Majeshi ya Ethiopia na Eritrea yanaelezwa kuzuia msaada wa chakula na mengineyo katika eneo hilo.
Akizungumza katika ibada ya Jumapili Papa Francis ametoa wito wa kusitisha mapigano katika eneo la Tigray.Umoja wa Mataifa na makundi ya misaada ya kiutu, unasema zaidi ya watu 350,000 katika eneo la Tigray wanakabiliwa na njaa na wengine milioni mbili wakitajwa wapo katika hatua mbaya zaidi, ikilinganishwa na baa la njaa la 2011 la Somalia.
Wakulima, wafanyakazi wa mashirika ya kutoa misaada na maafisa katika maeneo hayo wanasema chakula kimegeuzwa kuwa silaha ya kivita, ambapo wanajeshi wanakizuia au kukiiba.
