Friday, June 18, 2021

Mtoto aokotwa mtoni akielea ndani ya boksi India


Nahodha wa boti moja katika jimbo la India lililopo eneo la kaskazini la jimbo la Uttar Pradesh amepokea pongezi chungu nzima baada ya kumuokoa mtoto wa kike aliyepatikana akielea ndani ya boksi dogo katika mto Ganges.

Nahodha Gullu Chaudhary alisema kwamba alisikia kilio cha mtoto huyo mwenye siku 21 na kumpata amefungwa katika kitambaa chekundu ndani ya boksi lenye picha za mungu wa Kihindi.

Mtoto huyo amepelekwa hospitali na hali yake ya afya inachunguzwa kwa karibu. Atapelekwa katika nyumba ya mayatima baadaye.

Maafisa wanachunguza jinsi mtoto huyo alivyowekwa katika mto huo. Hawajashuku sababu za kutupwa kwa mtoto huyo , lakini tatizo la jinsia nchini India ni baya zaidi duniani.

Wanawake mara nyingi hubaguliwa kijamii na wasichana huonekana kama mzigo hususan katika familia masikini.

Ijapokuwa mimba nyingi changa za watoto wa kike hutolewa kwa usaidizi wa kliniki haramu na matukio ya watoto wa kike kuuawa ama kutelekezwa baada ya kuzaliwa ni ya kawaida.

Maafisa wa polisi walisema kwamba boksi hilo lilikuwa na kadi ya kuzaliwa kwake ambayo ilikuwa na muda wa kuzaliwa na tarehe na kutaja jina lake kama Ganga - Jina la Kihindi la Mto Ganges.

Serikali ya jimbo hilo imesema kwamba itasimamia gharama ya kumlea mtoto huyo.

Waziri kiongozi wa jimbo hilo Yogi Adityanath alitangaza kwamba mwendesha boti huyo atazawadia na serikali , ikiwemo kupatiwa nyumba kwa 'kuonesha utu'.

Maafisa katika wilaya ya Ghazipur , ambapo mtoto huyo aliokolewa , waliambia wanahabari kwamba hakimu wa wilaya hiyo MP Singh alimchunguza mtoto huyu huku maafisa wakitumwa kuonana na mwendesha dau huyo.

Bwana Chaudhary aliambia maripota kwamba wakati wakazi waliposikia kilio cha mtoto huyo kandakando ya mto,'' hakuna hata mtu mmoja aliyejitolea kusaidia. Lakini nilikimbia kumsaidia . Nilipofungua boksi hilo la mbao , nilimpata''.

Tukio hilo liliwavutia wengi ambapo kundi kubwa la watu lilikusanyika kandokando ya mto huo.

Kanda za video zilizochukuliwa katika eneo la tukio zilimuonesha mwendesha boti huyo akilichukua boksi hilo kutoka majini na kumbeba mtoto huyo katika mikono yake.

Baadaye alimchukua mtoto huyo na kumpeleka nyumbani kwake ambapo maafisa wa polisi walimchukua na baadaye maafisa wa kuangalia Watoto wakamchukua.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...