Tuesday, June 1, 2021

MRADI WA ADGG WAWANUFAISHA WAFUGAJI WA MIKOA 7

 

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), Prof. Erick Komba akisikiliza mada iliyokuwa ikiwasilishwa kuhusu mradi wa Uboreshaji na Uendelezaji wa Mbari za Ng'ombe wa Maziwa katika kikao kilichofanyika katika Makao Makuu ya Taasisi hiyo Jijini Dodoma.

Msimamizi Mkuu wa Mradi Uboreshaji na Uendelezaji wa Mbari za Ng'ombe wa Maziwa (ADGG), Dkt. Daniel Komwihangilo akifafanua jambo kuhusu mradi huo katika kikao cha tathmini kilichofanyika katika Ofisi za Makao Makuu ya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) Jijini Dodoma. Kulia ni Mshauri wa Mradi huo, Dkt. Maria Mashingo ambaye pia alishawahi kuwa Katibu Mkuu Mifugo.

Mratibu wa mradi wa ADGG, Dkt. Eliamoni Lyatuu akiwasilisha mada kuhusu mradi wa Uboreshaji na Uendelezaji wa Mbari za Ng'ombe wa Maziwa katika kikao kilichofanyika katika Makao Makuu ya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania Jijini Dodoma.

Picha ya pamoja ya Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), Prof. Erick Komba (aliyevaa suti nyeusi) na wajumbe wa kikao kilichofanya tathmini ya maendeleo ya mradi wa Uboreshaji na Uendelezaji wa Mbari za Ng'ombe wa Maziwa mara baada ya kumalizika kwa kikao hicho kilichofanyika katika Makao Makuu ya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania Jijini Dodoma.

***

Mradi wa uboreshaji na uendelezaji mbari za ng'ombe wa maziwa (ADGG) ambao umefanyika katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Iringa, Mbeya Njombe, na Songwe wawanufaisha wafugaji katika maeneo hayo.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), Prof. Erick Komba (31.05.2021) baada ya kumalizika kwa kikao cha tathmini ya maendeleo ya mradi huo ambao kwa hapa Tanzania unafanyika katika mikoa saba (7) na Halmashauri ishirini nan ne (24).

Prof. Komba amesema mradi huo ulikuwa ni wa miaka sita na unatarajiwa kumalizika mwaka 2022 mwezi wa nne. Lengo la kikao hicho cha tathmini ilikuwa ni kuangalia mazuri yaliyofanyika kupitia mradi na namna gani yanaweza kuendelezwa ili wafugaji waendelee kupata tija na kukuza kipato ufugaji.

"Wafugaji wamenufaika sana kutokana na uwepo wa mradi huu kutokana na ushauri mbalimbali waliokuwa wakiupata kutoka kwa wataalamu juu ya nini cha kufanya pale mifugo yao inapopata matatizo na aina gani ya mbegu bora za ng'ombe wa maziwa wanatakiwa kufuga," alisema Prof. Kombe.

Katika kikao hicho pia wamejadili namna ya kuwashirikisha wadau mbalimbali ambao watasaidia kuendeleza kazi zilizofanywa na mradi ili ziwe kuwa endelevu ikiwepo serikali, wadau wa maziwa na wadau wa mawasiliano.

Lengo ni kuhakikisha uzalishaji wa maziwa unaongezeka hapa nchini na hivyo kupunguza uagizaji wa maziwa kutoka nje ya nchi na hivyo kumnufaisha mfugaji wa hapa nchini kwa kukuza kipato chake.

Naye Mshauri wa Mradi wa kuendeleza mbari za ng'ombe wa maziwa, Dkt. Maria Mashingo ambaye pia alishawahi kuwa Katibu Mkuu Mifugo amesema mradi huu ni muhimu sana katika kuleta mageuzi kwenye sekta ya maziwa kwa kuhakikisha kuna kuwa na mbegu au vizazi bora vya ng'ombe ambao wanauwezo mkubwa wa kutoa maziwa mengi.

Dkt. Mashingo amesema mradi huu umetekelezwa kwa kutumia mbinu kubwa ambayo katika Sekta ya Mifugo haijawahi kufanyika kwani kinachofanyika ni pamoja na utambuzi wa ng'ombe kwa kujua uzazi na ubora wake.

Hivyo ameshauri itafutwe njia ya kuhakikisha matokeo ya mradi huu yanaendelezwa kwani watafiti wamefanya kazi kubwa ambayo imeleta tija kwa wafugaji kwa kuongeza uzalishaji wa maziwa na kuongeza kipato chao.

Msimamizi Mkuu wa Mradi wa ADGG, Dkt. Daniel Mwakihangilo amesema wamekuwa wakiwashauri wafugaji juu ya matumizi ya mbegu bora za ng'ombe wa maziwa ikiwa ni pamoja na matumizi ya madume bora ambayo yanapatikana katika maeneo wanayoishi na kwa kutumia njia ya uhimilishaji ili wapate ng'ombe wenye uwezo wa kutoa maziwa mengi.

Mratibu wa mradi wa ADGG na Mtafiti wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Duniani, Dkt. Eliamoni Lyatuu amesema kwanza walikuwa na lengo la kuwa na mfumo wa ukusanyaji wa taarifa za mifugo, pili kuweza kurejesha mrejesho kwa wafugaji pale wanapokuwa na maswali au maoni na tatu ni kuipanga mifugo kulingana na ubora wake ili kuwasaidia wafugaji kupata mifugo sahihi yenye uwezo wa kutoa maziwa mengi.

Akizungumzia kuhusu mradi huu, Bi. Yusta Elisha ambaye ni mfugaji wa ng'ombe wa maziwa amesema kupitia mradi wa ADGG wameweza kupata maelekezo juu ya ufugaji bora, wamekuwa wakipata ujembe kupitia simu juu ya namna ya kuendeleza shughuli zao za ufugaji ambazo zimewasaidi kuongeza uzalishaji wa maziwa tofauti na kiwango cha maziwa walichokuwa wakikipata kipindi cha nyuma ambapo kwa sasa wanapata lita 20 kwa siku tofauti na lita kumi walizokuwa wakipata kabla ya mradi.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...