Meli kubwa kabisa ya jeshi la wanamaji la Iran imeteketea na baadae kuzama hii leo katika mazingira yasiyoeleweka kwenye ghuba ya Oman.
Hayo yameripotiwa na mashirika ya habari ambayo hayamilikiwi moja kwa moja na serikali. Mashirika hayo ya Fars na Tasnim yameeleza kwamba juhudi za kuiokoa meli ya Kharg zimeshindwa.
Kwa mujibu wa taarifa za kituo cha televisheni ya taifa wazima moto walijaribu kuudhibiti moto huo. Meli hiyo iliyopewa jina la kisiwa ambacho ndio kituo kikubwa cha mafuta cha Iran,Kharg, ilizama karibu na bandari ya Jask kiasi kilomita 1,270 Kusini mashariki mwa Tehran katika ghuba ya Oman karibu na mlango bahari wa Hormuz.
Picha zinazosambaa katika mitandao ya kijamii nchini Iran zinaonesha mabaharia wakiwa wamevaa jaketi za kujiokoa wakiondoka kwenye meli hiyo huku moto ukiwaka.