Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini Dkt Benson Ndiege ameagizwa kumsimamisha kazi Kaimu Mrajis Msaidizi wa Vyama Vya Ushirika Mkoa wa Lindi Ndg Edmund Masawe.
Edmund amesimamishwa kazi kutokana na kukilazimisha Chama cha Ushirika wa mazao (AMCOS) cha Umoja kilichopo Wilaya ya Liwale Mkoani Lindi kukodi ghala kwa ajili ya kuhifadhia Korosho ilihali chama hicho kina ghala lake la kuhifadhia korosho.
Waziri wa Kilimo Mhe Prof Adolf Mkenda ametoa agizo hilo tarehe 13 Mei 2021 wakati akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake Jijini Dodoma.
Mhe Mkenda amemtaka Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini Dkt Benson Ndiege kujitathmini kutokana na kushindwa kutekeleza ahadi ya kutoa ushauri wake alioelekezwa wakati wa kikao cha majadiliano kilichofanyika tarehe 8 Mei 2021.
Waziri Mkenda amebainisha kuwa katika kikao kazi hicho Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini aliagizwa kutoa taarifa ya ushauri wake kuhusu Mradi wa pamoja wa vyama 32 vya msingi vya Ushirika (G32) vya Mkoani kilimanjaro lakini hakufanya hivyo.
"Katibu Mkuu Mimi nadhani Mrajis wa Vyama vya Ushirika anafanya mzaha, Anadhani siwezi kumng'oa na pengine mahali pa kuanza kupafumua katika Wizara ya Kilimo ni Tume ya Maendeleo ya Ushirika" amesema Mhe Mkenda
Prof Mkenda amesema kuwa amemuweka Mrajis na mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya ushirika katika uangalizi maalumu huku akimuagiza kufika Jumatatu tarehe 17 Mei 2021 kuwasilisha mapendekezo hayo haraka iwezekanavyo.
Waziri Mkenda amesema kuwa amekabidhiwa kuingoza Wizara ya Kilimo ili kuimarisha sekta ya Ushirika nchini ikiwa ni pamoja na kuongeza uzalishaji na tija kwa wakulima.