WANAFUNZI 200 katika Wilaya ya Magu mkoani Mwanza wamepata mimba katika kipindi cha Januari,2020 hadi Machi mwaka huu.
Mkuu wa Dawati la Jinsia wilayani Magu, Amani Migoha, aliliambia HabariLEO katika mazungumzo kuwa Januari hadi Desemba, 2020kulikuwa na wananfunzi 111 waliopata mimba na tangu Januarihadi Machi mwaka huu, wanafunzi 71 wamebainika kupata mimba.
Migoha alisema tatizo la mimba za utotoni bado ni changamoto katika wilaya yao.
Aliwataka wazazi kuhakikisha wanafuatilia mwenenedo wa watoto wao katika elimu.
Mkuu wa Kituo cha Polisi Wilaya ya Magu, Mahmoud Banda, alisema watuhumiwa wengi wa mimba wamekuwa wakitoroka baada ya kusikia wanatafutwa na Jeshi la Polisi.
Alisema kumekuwepo na tatizo la wazazi kuzungumza na wahusika wanaowapa watoto wao mimba na wanaposhindwana, ndipo wazazi na walezi hao huamua kukimbilia polisi kuhitaji msaada wa kisheria.
Kwa mujibu wa uchunguzi, hali hiyo huchangia kwa kiasi kikubwa kuharibu na kupoteza ushahidi huku pia ikitoa mwanya kwa watuhumiwa kujiandaa na kutoroka kirahisi.
Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salum Kalii, alisema wenyeviti wa vijiji na vitongoji wahakikishe wanafuatilia mahudhurio ya watoto wote ili kubaini watoro na kujua sababu za utoro huo.
