Na John Walter- Manyara
Klabu ya waandishi wa habari wa Mkoa wa Manyara (MPC) imeadhimisha siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani kwa kutoa msaada wa vyakula kwa kituo cha watoto cha watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu (MAHOCE) na kituo cha wazee cha Sarame Kata ya Magugu Wilayani Babati.
Mwenyekiti wa Klabu Zacharia Mtigandi amesema wametoa msaada huo ili kushiriki pamoja madhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari na watoto na wazee hao ili kuwapa faraja.
Ntigandi amesema MPC iliamua kuadhimisha siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani kwa kushiriki na watoto na wazee hao ikiwa ni mchango wao katika kusaidia makundi hayo yenye uhitaji.
Waandishi hao katika kituo cha Manyara Holistic Centre (MAHOCE) mjini Babati wametoa mchele kilo 100 pamoja na mafuta ya kupikia lita 20.
Aidha kwenye kituo cha wazee Sarame waliwapatia mchele kilo 50, lita 20 za mafuta na viburudisho.
Mkurugenzi wa MAHOCE Joshua Johnson amewashukuru waandishi hao wa habari kwa kuwatembelea na kuwapa msaada huo wa vyakula kwenye madhimisho hayo ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari.
Amesema wanawahudumia takribani watoto 80 katika kituo hicho kilichoanzishwa mnamo mwaka 2007 na kina watoto 80.
Pamoja na hayo klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Manyara, wamezindua Blog ya chama ambayo itatoa fursa kwa waandishi kuutangaza mkoa kupitia taarifa zao watakazokuwa wanazichapisha na kuingiza kipato kupitia matangazo mbalimbali.
Makamu Mwenyekiti wa MPC, Mary Margwe amesema kwa kipindi hiki wameadhimisha tofauti na miaka iliyopita ambapo walikuwa wanakutana na wadau mbalimbali wa habari wa mkoa huo.