Nahodha John Raphael Bocco amefunga mabao mawili Simba SC ikiibuka na ushindi wa 3-0 dhidi ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini katika mchezo wa marudiano wa Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika jioni ya leo Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Pamoja na ushindi huo, Simba SC imetolewa baada ya kuchapwa 4-0 katika mchezo wa kwanza Jumamosi iliyopita Jijini Johannesburg, Afrika Kusini.
Bocco alifunga mabao yake dakika za 24 akimalizia pasi ya mshambuliaji Mkongo, Chris Kope Mugalu na dakika ya 56 akimalizia krosi ya kiungo wa kimataifa wa Msumbiji, Luis Jose Miquissone.
Bao la tatu la Simba limefungwa na kiungo Mzambia, Clatous Chota Chama baada ya juhudi zake mwenyewe kabla ya kufumua shuti kali.
Simba SC ingeweza kuondoka na ushindi waliouhitaji kama safu yake ya ushambuliaji ingetumia vyema nafasi zote walizopata.
Wekundu wa Msimbazi Simba walihitaji ushindi wa mabao 5-0 ili kujihakikishia nafasi ya kufuzu hatua ya nusu fainali kwa mara ya kwanza lakini imeshindikana.
Mwaka 1997 klabu ya Simba ili pindua matokeo na kusonga mbele kwenye michuano hii ya vilabu barani Afrika dhidi ya Mufurila Wonders ya Zambia ambapo mchezo wa kwanza Simba ilifungwa bao 4-0 lakini mchezo wa pili walipindua matokeo na kushinda 5-0 na kusonga mbele.