Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeanza kutenga maeneo ya kupanda mbegu za malisho ya kisasa aina ya Juncao lengo likiwa ni kuwa na maeneo ya kutosha kwa ajili ya kupanda mbegu hizo ambazo zitasambazwa kote nchini ili kutatua changamoto ya malisho.
Hayo yalisemwa na Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, anayeshughulikia mifugo, Prof. Elisante Ole Gabriel alipotembelea kukagua eneo ambalo limetengwa kwa ajili ya kupanda mbegu hiyo ya Juncao katika Shamba la kuzalisha malisho ya mifugo la Vikuge lililopo Mkoani Pwani Mei 17, 2021.
Prof. Ole Gabriel alisema kwa kuanzia katika shamba hilo la Vikuge wametenga Ekari Arobaini (40) kwa ajili ya kupanda mbegu hizo na zitasambazwa katika Halmashauri zote nchini ili malisho hayo yaweze kuzalishwa kwa wingi jambo ambalo litapelekea kupatikana kwa urahisi.
"Tumepanga kutumia eneo la Wizara lililopo Mkoani Simiyu linaloitwa Shishiu, na Langwira ambalo lipo Mkoani Mbeya haya maeneo yote tutayatumia kupanda haya malisho ili yapatikane kwa wingi na yasambazwe katika Halmashauri nyingi nchini," alisema Prof. Ole Gabriel
Alisema kuwa Serikali itaendelea kufanya kila linalowezekana kuhakikisha changamoto ya malisho inakwisha na kubaki historia, huku akiwaomba wafugaji kuthamini hatua hizo zinazochukuliwa na Serikali ili kusaidia lengo hilo kufanikiwa haraka iwezekanavyo.
Aliongeza kuwa lengo la Rais, Mama Samia Suluhu Hassan ni kuona sekta ya mifugo inachangia katika kukuza uchumi wa nchi, hivyo malisho hayo yakisimamiwa vizuri yatakuwa ni chanzo kipya cha mapato na kuchangia kukuza uchumi wa nchi.
"Tunategemea ifike mahali tuanze kuuza kwa wingi malisho tutakayozalisha nje ya nchi na kwa kufanya hivyo tutapata fedha za kigeni ambazo zitasaidia sana kukuza uchumi wa wananchi wetu na nchi kwa ujumla," alifafanua Prof. Ole Gabriel
Aidha, alitumia fursa hiyo kuwataka Makatibu Tawala kushiriki vyema katika kampeni hiyo ya kuzalisha malisho katika maeneo yao akisema kuwa jambo hilo linagusa moja kwa moja wananchi walio katika maeneo yao hivyo hawana budi kuhakikisha wanafanikisha jitihada hizo.
Prof. Ole Gabriel alisema kuwa lengo la Serikali sio kufanya biashara ya mbegu hiyo bali kuhakikisha inasambazwa kwa wafugaji wote nchini ikiwemo mashamba ya malisho ya mifugo ya serikali ili kutatua changamoto iliyopo ya uhaba wa malisho.
Aliongeza kwa kusema kuwa kando na majani hayo kuwa na faida nyingi kwa mifugo pia yana matumizi mengine mengi ikiwemo kutengenezea nishati, kutunza mazingira hususan kuzuia mmomonyoko wa ardhi, na nchi ya china wanatumia kuzalisha uyoga.