Thursday, May 13, 2021

RC Mahenge aagiza TAWA, TANAPA na Halmashauri ya Chamwino kushirikiana kutatua kero ya Tembo wanaharibu mazao na kuua watu kijiji cha Ilangali


Na Ezekiel Mtonyole – Dodoma.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt Binilith Mahenge ameiagiza Mamlaka ya usimamizi Wanyama pori Tanzania TAWA, Mamlaka ya hifadhi ya taifa TANAPA Ruaha na halmashauri ya Wilaya ya Chamwino kushirikiana mara moja kuwadhibiti tembo waliovamia katika Kijiji cha Ilangali kata ya Manda na kuharibu mazao, kujeruhi na kuua.

Dkt Mahenge ametoa agizo hilo katika Kijiji hicho kilichopo Wilaya ya Chamwino alipofika kwa lengo la kusikiliza kero za wananchi, kisha kuibuka kwa suala hilo ambapo wananchi wamesema tembo hao sasa imekuwa kero kubwa katika Kijiji hicho na kusababisha hawalali kabisa kwa kulinda mazao yao.

Ambapo ameagiza TAWA, TANAPA na halmashauri ya Wilaya kwa kushirikisha serikali ya mtaa wakae mara moja kutatua changamoto hiyo kwa dharua huku wakiweka mipango endelevu yakuzuia wanyama hao waharibifu kuto ingia katika mashamba ya wananchi.

"Nataka mshirikiane muweke mikakati shirikisheni serikali ya mtaa wekeni afisa wanyapori mwenye silaha atakayeweza kutatua changamoto kwa dharura inapotokea tembo kaingia shambani tatizo hap ani kubwa" amesema Dkt Mahenge.

Pia Dkt Mahenge amezitaka Mamlaka hizo kuhakikisha zinatoa elimu ya kutosha kwa wananchi namna ya kujilinda wenyewe na Wanyama hao pindi maafisa wanapokuwa mbali na eneo hilo kwani litasaidia kupunguza madhara yatokanayo na kujeruhiwa au kuuawa kwa wananchi hao.

Dkt Mahenge amezitaka mamlaka hizo kuharakisha kuunda vikundi maalumu na kuvipa elimu ya kutosha ya namna ya kukabiliana na wanyama hao ambavyo pia vitapewa mafunzo kuhakikisha vinatoa msaada wa dharura.

Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Bi Vumilia Nyamoga amesema tayari wameshachukua hatua ambapo wamepeleka andiko ofisi ya Katibu Tawala Mkoa ili kupewa afisa wanyamapori atakayepewa vitendea kazi vyote na atakaa katika Kijiji hicho ili kusaidia kutoa msaada wa haraka inapotokea tembo wameingia mashambani.

Kwa upande wake Kaimu Kamishna msaidizi mwandamizi wa TAWA kanda ya kati Pascal Mrina amekiri kutokea kwa vifo na baadhi kujeruhiwa na tembo hao na kubainisha kuwa tayari wamejipanga kukabiliana na vitendo hivyo ambapo wanatafuta afisa ambae atakuwa katika eneo hilo maalumu.

"Ni kweli matukio hayo yametokea na ofisi yangu ilipata taarifa hasa msiba wa mwezi wa nne hata mimi nimefika hapa kushirikiana na wananchi, shida hapa hakuna afisa wanyamapori kwa kuna askari wachache ukizingatia tunahudumia kanda nzima na maeneo yanayovamiwa ni mengi" amesema.

Nae Afisa mhifadhi mwandamizi wa TANAPA, Ruaha Sharif Abdul amesema tatizo la wanyama kuvamia maeneo ya watu ni tatizo katika wilaya zote zinazopakana na mbuga hiyo ikiwamo Chamwino, Iringa, Mbalali na Chunya, huku akibainisha kuwa kwa Chamwino ni kubwa kuliko.

Amesema kati ya Wilaya hizo vijiji takribani 38 vinavamiwa mara kwa mara na kuleta madhara kwa wananchi na kwa kulitambua hilo tayari wameanza kutumia mkakati uliozinduliwa 2020 wa namna ya kutatua msuguano kati ya wananchi na Wanyama, wanatarajia kuanza kutoa elimu kwa vikundi maalumu kwa ajili ya kukabiliana na Wanyama hao.

"Mwanzo tulikuwa na vikundi vya kuzuia ujangili sasa tunaweza kutumia vikundi vilevile au tukaunda vikundi vingine na tukawapa elimu ya kukabiliana na Wanyama hao ambapo tutawawezesha vitendea kazi pia" amesema.

Katika hatua nyingine Dkt Mahenge ameiagiza Wakala wa  barabara za miji na vijijini TARURA kuhakikisha inakarabati barabara inayoingia katika kata ya Manda hadi kijijini hapo ambayo inaurefu wa kilomita 69 kwa kuwa imeharibika sana.

"Wote mashahidi tumekuja na barabara hii ni mbovu sana ukizingatia tunalengo la kuweka lango la utalii hapa, lazima hii bara bara ikarabatiwe haraka iwezekanavyo na katika ukarabati huo uanzie hapa kurudi mjini na hili nitalifuatilia mwenyewe" amesema.

 

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...