Mkuu wa wilaya ya Kahama Mhe. Anamringi Macha akizungumza leo Jumatatu Mei 3,2021 wakati wa Maadhimisho siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Mkoa wa Shinyanga yaliyofanyika katika Manispaa ya Kahama
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mkuu wa wilaya ya Kahama Mhe. Anamringi Macha amewataka waandishi wa habari kuilinda tasnia ya habari kwa kuhakikisha wanawaondoa waandishi wa habari vishoka 'makanjanja' ambao wamekuwa wakiharibu taswira ya tasnia hiyo kwa kuandika na kusambaza habari za uongo 'Fake News'.
Mkuu huyo wa wilaya ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Mei 3,2021 wakati wa Maadhimisho siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Mkoa wa Shinyanga yaliyofanyika katika Manispaa ya Kahama yakiongozwa na kauli mbiu ni 'Habari kwa Manufaa ya Umma' yaliyoandaliwa na Klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga (Shinyanga Press Club – SPC) na kuhudhuriwa na wadau wa habari mkoa wa Shinyanga.
"Tasnia ya Habari sasa imeingiliwa, na inataka kuonekana haiheshimiki. Ndani yenu wamo vishoka wanaandika na kusambaza taarifa ambazo siyo sahihi na wenye jukumu la kuilinda tasnia hii ya habari ni nyinyi waandishi wa habari.
Pamoja na uhuru uliopo lakini na nyinyi tunaomba mtusaidie kuwaondoa vishoka katika tasnia ya habari maana kila wakati tunaona habari za uongo 'Fake News'. Sisi kama serikali tupo tayari kushirikiana nanyi kuwabaini vishoka",amesema Macha.
"Tusikubali watu wasio na uelewa na masuala ya uandishi wa habari wavamie tasnia hii. Ili kujenga heshima ya taaluma ya habari wilayani Kahama naomba nipewe orodha ya waandishi wa habari waliopo Kahama na mkoa wa Shinyanga kwa ujumla ili mwandishi anapofika ofisini kwangu nijue kama taarifa tunazotoa zinatolewa kwa mwandishi sahihi",ameongeza Macha.
Macha amewasisita waandishi wa habari kuandika habari sahihi kwa manufaa ya umma huku akivisihi vyombo vya habari kuandika habari za uchunguzi badala ya kutoa tu taarifa.
"Vyombo vya habari vina fursa ya kuchangia masuala mbalimbali yanayohusu jamii, tunachokiomba tuwe na uandishi unaojenga, uandishi wenye staha. Na nyie waandishi wa habari andikeni mazuri tunayofanya, andikeni ya kutukosoa, andikeni kwa staha, habari ilenge kufundisha, kutoa taarifa na hakikisheni uandishi wenu unakuwa wa kizalendo,kulinda nchi na wa staha",amesema Macha.
Pia amezitaka taasisi za umma kutoa ushirikiano kwa waandishi wa habari zitambue vyombo vya habari vilivyopo katika maeneo yao na kutoa taarifa mbalimbali ili kuepusha waandishi wa habari kuandika taarifa zisizo sahihi kwani wakati mwingine wanapokosa ushirikiano waandika taarifa wanazoziona ambazo wakati mwingine zinakuwa siyo sahihi.
Aidha amewataka waandishi wa habari kuendelea kutoa taarifa kwa kujiridhisha kwa pande zote mbili na wazingatie kuandika habari kwa usahihi na kutoyaacha nyuma masuala ya kiuchumi.