Thursday, May 20, 2021

MBUZI 17 WATAFUNWA NA FISI LUBAGA..AFISA MIFUGO ATEKETEZA MABAKI YA NYAMA KWA MOTO

Wakazi wa Kata ya Lubaga halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga Mkoani Shinyanga wameiomba serikali kuwasaidia kutatua changamoto ya uwepo wa wanyama aina ya  fisi kwenye maeneo yao baada ya fisi hao kuvamia zizi na kuua mbuzi 17 na kondoo katika familia ya Monica Paul mkazi wa mtaa wa Azimio kata ya Lubaga.

Ndugu wa familia ya Monica Paul wameiambia Malunde 1 blog kuwa ilikuwa majira ya saa kumi usiku wa kuamkia Jumatano Mei 19,2021 ndipo waliposikia mlio wa fisi hali iliyo walazimu kutoka nje na baada ya kutoka nje ndipo walipogundua kuwa mbuzi wa wameliwa na fisi hao.

Wakazi wa eneo hilo wamesema kuwa kwa sasa fisi hao wamekuwa wakionekana mara kwa mara katika maeneo yao tofauti na ilivyokuwa siku za nyuma.

Diwani wa kata ya Lubaga Reuben Dotto ameeleza kuwa  changamoto ya uwepo wa fisi kwenye maeneo yao imesababisha hofu kwa wananchi na kusababisha baadhi ya wanafunzi kushindwa kuhudhuria shuleni mapema wakihofia kuumwa na fisi

Afisa mifugo wa kata ya Lubaga Eliaremisa Mbise amethibitisha
 kutokea kwa tukio hilo na kuagiza wakazi wa kata hiyo kuteketeza kwa moto  masalia ya mbuzi waliouawa na fisi ili kuzuia athari zinazoweza kujitokeza kutokana na baadhi ya wakazi wa eneo hilo kula mbuzi walioliwa na fisi.

Mbuzi akiwa ameuawa na fisi
mabaki ya mbuzi

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...