Jeshi la Burkina Faso limesema leo kuwa limewauwa wale lililowataja kuwa magaidi wasiopungua 20, na kuharibu ngome zao nne kwenye operesheni ya pamoja katika mikoa mwili ya kaskazini iliyokumbwa na uasi wa wapiganaji wa itikadi kali.
Taarifa ya jeshi hilo imesema operesheni hiyo ilianzishwa Mei 5 kwenye mikoa ya Nord na Sahel, ikivihusisha vikosi vya kawaida na maalumu, jeshi la anga na kitengo cha polisi kilichoko chini ya kamandi ya jeshi.
Chanzo kutoka jeshi kimeliambia shirika la habari la AFP, kwamba operesheni hiyo iliyopewa jina la Houne - au Heshima kwa lugha ya Fula, inatarajiwa kudumu kwa zaidi ya mwezi mmoja.
Vikosi vya jeshi vimetoa matangazo mengi kuhusiana na operesheni kama hizo huko nyuma, lakini vinashindwa kudhibiti maafa yanayoongezeka yanayosababishwa na wapiganaji wa itikadi kali nchini humo.
Takribani watu 1,300 wamekufa na zaidi ya milioni moja wameyakimbia makaazi yao.
