Asasi ya kimataifa inayoshughulikia wakimbizi wa ndani IDMC imesema katika ripoti yake kwamba watu zaidi ya milioni 40 mnamo mwaka uliopita walilazimika kuyahama makaazi yao kutokana na kuongezeka kwa migogoro na pia kutokana na hali isiyoeleweka ya tabia nchi.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo inayotolewa kila mwaka zaidi ya asilimia 80 ya watu hao walikumbwa na hali hiyo kwenye mabara ya Afrika na Asia.
Hii ni mara ya sita kwa kituo hicho kutoa ripoti hiyo. Asasi hiyo ya kimataifa imesema mwaka jana watu zaidi ya milioni 30 walitimuliwa kutoka kwenye makazi yao kutokana na dhoruba, mafuriko, mioto ya porini na ukame.
Hali hiyo imesababisha wasiwasi miongoni mwa wanasiasa katika nchi tajiri juu ya kuongezeka kwa wahamiaji kutoka nchi masikini. IDMC inakadiria kwamba watu nusu milioni wamekimbia kutoka jimbo la Tigray nchini Ethiopia kutokana na vita mwaka uliopita.
Hata hivyo, tangu wakati huo Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia Watoto, UNICEF limekadiria kuwa idadi hiyo imeongezeka na kufikia zaidi ya milioni moja.