Sunday, April 25, 2021

Yametiamia: Ummy awatumbua Mkurugenzi Temeke, Sumbawanga



Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Ummy Mwalimu amewasimamisha kazi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Lusubilo Mwakabibi na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, Nyangi John Msemakweli baada ya kupokea malalamiko na tuhuma za mwenendo usiofaa.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Ummy Mwalimu
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Tamisemi, Waziri Ummy ametoa agizo hilo leo Aprili 25, 2021 huku akitaja sababu nyingine ya kusimamishwa kwa Mkurugenzi huyo kuwa ni matumizi mabaya ya madaraka.

"Waziri Ummy amemsimamisha kazi Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Lusubilo Joel Mwakabibi baada ya kupokea malalamiko na tuhuma za mwenendo usiofaa, matumizi mabaya ya madaraka, ubadhirifu na usimamizi usiorihisha wa miradi ya maendeleo katika halmashauri ya Manispaa ya Temeke kutoka kwa wananchi, viongozi na vyanzo vingine.

"Kufuatia tuhuma hizo, waziri Ummy amemuagiza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais –TAMISEMI kupeleka timu za uchunguzi mara moja," imeeleza taarifa hiyo.

Ikumbukwe kwa kipindi kirefu mKurugenzi huyo wa Temeke amekuwa wakilalamikiwa na wananchi ikiwamo vyombo vya habari kwa kutoa lugha na matamshi yasiyofaa.

Pia Waziri Ummy amemsimamisha kazi Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, Nyangi John Msemakweli kutoka na tuhuma za ubadhirifu usimamizi mbovu wa miradi ya maendeleo na mahusiano yasiyoridhisha na Madiwani, Mkuu wa Wilaya na Viongozi wengine wa Wilaya na Mkoa wa Rukwa.

Aidha, Waziri Ummy amewaelekeza wakuu wa Mikoa wote kusimamia vyema shughuli za maendeleo na utekelezaji wa miradi kwenye mikia yao.

Paia amewataka wakurugenzi na watendaji wote wa Halmashauri kuheshimu mipaka yao ya kazi na kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na amewaasa kuwa serikali haitasiata kuchukua hatua za kisheria na kinidhamu kwa watumishi watakaobainika kufanya ubadhirifu na kukiuka Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...