Spika wa Bunge, Job Ndugai amewataka wabunge kutovaa tai nyekundu leo jioni Alhamisi Aprili 22, 2021 wakati Rais Samia Suluhu Hassan akilihutubia Bunge kwa kuwa rangi hiyo huvaliwa na wenye mamlaka.
Amesema ikiwa mbunge atavaa tai nyekundu atazuiwa kuingia katika ukumbi wa chombo hicho cha kutunga sheria.
Ameeleza hayo leo wakati akiahirisha kikao cha asubuhi kupisha maandalizi ya ujio wa rais bungeni na kubainisha kuwa kwa kuwa rangi hiyo huvaliwa na wenye mamlaka, mwenye mamlaka atakuwa bungeni leo
"Katika kipindi cha leo haitapendeza mbunge kuvaa tai nyekundu kwa sababu rangi hiyo ni kwa wenye mamlaka. Waheshimiwa wabunge kama mnavyofahamu leo jioni rais atakuwa nasi hapa lakini kama tulivyozoea na kwa utamaduni wa kawaida wale wenzangu na mimi tusivae tai nyekundu, na kama ukija nayo watakurudisha pale getini,"amesema Ndugai.
Ndugai aliahirisha shughuli za Bunge saa mbili kabla ya muda uliopangwa akisema ukumbi unatakiwa kufanyiwa maandalizi ikiwemo ukaguzi wa kila kiti.