BAADA ya Simba kushinda mechi zote mbili za Kanda ya Ziwa, hivi karibuni, kocha msaidizi wa timu hiyo, Selemani Matola amesema mchezo wa leo dhidi ya Gwambina FC timu yake itacheza kama fainali ili waweze kushinda michezo yote ya ukanda huu.
Mara baada ya kuifunga Kagera Sugar, juzi Jumatano mkoani Kagera, Matola alifunguka:
"Tunashukuru kwa kupambana na kupata matokeo mbele ya Kagera Sugar, haikuwa kazi rahisi."Kwa sasa tunakwenda kufanyia kazi mapungufu yaliyoonekana katika mchezo huu ili mchezo ujao dhidi ya Gwambina tuweze kufikia malengo ambayo tunahitaji."
Tumepanga kucheza kama fainali kwa kuwa malengo yetu ni kupata alama zote 9 katika michezo mitatu ya Kanda ya Ziwa, tunajua hautakuwa mchezo rahisi kutokana na Gwambina kupata matokeo mabovu katika michezo iliyopita lakini tutapambana.
"Kwa sasa Simba inakabiliwa na michezo ya mara kwa mara nadhani kila baada ya siku mbili tunapaswa kucheza, ndiyo maana umeona huku Kagera baada ya kupata mabao mawili tukaamua kucheza soka bila kutumia nguvu nyingi."
STORI: JOHNSON JAMES, Mwanza