Tuesday, April 13, 2021

Jinsi Misri ilivyomdai mamilioni ya dola mmiliki wa meli iliyoziba mfereji wake muhimu Suez


Meli ya kubeba mizigo ya urefu wa takriban mita 400 kwa jina Ever Given ilikwama kimshazari katika mfereji wa Suez Machi 23 kwa karibu wiki moja na kufunga moja ya njia yenye shughuli nyingi za kibiashara duniani.

Mafanikio ya kuondoa meli hiyo iliyokuwa imekwama katika mfereji wa Suez mwisho wa mwezi Machi yalifurahikiwa kote duniani wengi wakifikiria kuwa sasa suala hilo limefika mwisho.

Lakini kinachooneka ni kwamba bado ufumbuzi wa suala hili uko mbali kupatikana.

Je hilo ni kwasababu gani? Misri imeamua kuwa haitaruhusu meli hiyo kuondoka - hadi pale itakapolipa faini ya dola bilioni moja kama fidia ya hasara iliyopatikana kipindi hicho chote cha wiki moja.

"Meli hiyo itasalia hapa hadi uchunguzi utakapokamilika na fidia kulipwa," Osama Rabie, Rais wa Mamlaka ya Mfereji wa Suez (ACS), amearifu televisheni ya taifa nchini Misri.

Ni matumaini yetu makubaliano ya haraka tayafikiwa," aliongeza. "Pindi tu watakapokubaliana katika suala la fidia, meli hiyo itaruhusiwa kuondoka."

Kiwango cha fidia ya kulipwa, mwanzoni mwa Aprili Rabie alisema kuwa "hasara iliyosababishwa pamoja na gharama ya mashine iliyotumika kuirejesha meli hiyo kwenye njia yake, zote zitahesabiwa."

"Makadirio yake yatafika dola bilioni 1 za Marekani au pengine hata zaidi kidogo. Hii ni haki ya Misri," amesema.

Kima hiki cha pesa kitahesabiwa kulingana na ada ya usafiri iliyopoteza, hasara iliyopata wakati inatengeneza njia, juhudi za kuivuta meli hiyo na gharama za vifaa na nyenzo zilizotumika.

Shoei Kisen, kampuni moja ya Japani ambayo ndio mmiliki wa meli ya Ever Given, imesema kuwa bado haijapokea madai rasmi au ya kisheria yanayozungumzia kulipwa kwa fidia kwasababu ya hasara iliyosababishwa na kukwama kwa meli hiyo, lakini wanachojua ni kwamba wako katika mazungumzo na mamlaka inayosimamia njia hiyo ya usafirishaji.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...