Na Omary Mngindo, Chalinze
UONGOZI wa Halmashauri ya Chalinze Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani, umeandaa dua Maalumu la kuiombea Taifa, linalotaraji kufanyika Jumatano ya Aprili 7.
Dua hiyo inataraji kuwahusisha viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini wakiwemo wa kisiasa, litafanyika kwenye ukumbi wa Mikutano kwenye Halmashauri hiyo kuanzia saa 3 asubuhi mpaka saa 7 mchana.
Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Geofrey Kamugisha, akizungumza na Waandishi wa habari kwenye ofisi za Halmashauri hiyo, ambapo alisema dua hiyo pia litatumika kumkumbuka Hayati John Magufuli, aliyefariki dunia Machi 17 mwaka huu.
"Sanjali na hilo pia dua hiyo tutamtakia afya njema Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan, na viongozi mbambali ili waendelee kuwatumikia wananchi, hatimae tufikie malengo tuliyojiwekea," alisema Kamugisha.
Aliongeza kuwa nchi kwa mara ya kwanza imepata pigo la kuondokewa na Rais aliyekuwa madarakani, hivyo wanakila sababu ya kuendelea kumuomba Mwenyeezimungu azidishe wa-Tanzania moyo wa subira katika kipindi hiki.
"Tunaendelea kumuomba Mwenyeezimungu kwa kutupatia moyo wa subira katika kipindi hiki kigumu, nasi Halmashauri tumeandaa dua maalumu kumuombea Rais wetu Mama Samia sanjali na viongozi ngazi zote wakiwemo wananchi wa Chalinze," alisema Kamugisha.
Aidha amewaomba viongozi wa dini na wa kisiasa kuwahimiza wananchi kufika kwa wingi katika dua hilo, linalotaraji kuanza saa tatu asubuhi ili kwa pamoja washirikiane kuliombea taifa liendelee kuwa la amani, upendo na utulivu.
Source