KIKOSI cha klabu ya soka ya Namungo kinaendelea na mazoezi ya kujiandaa na mchezo wao wa tatu, wa hatua ya makundi ya kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Nkana ya Zambia utakaopigwa Ijumaa ya Aprili 2, kwenye uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.
Namungo itaingia katika mchezo huo ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kupoteza michezo yao miwili ya kwanza ya hatua ya makundi, ambapo walifungwa bao 1-0 dhidi ya Raja Casablanca ya Morocco, na kukubali kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya Pryamids ya Misri.
Namungo mpaka sasa inakamatia nafasi ya tatu kwenye msimamo wa kundi D la michuano hiyo ikiwa bado haijapata alama yoyote.
Pyramids na Raja Casablanca ndiyo vinara wa msimamo na pointi zao sita, huku Nkana wao wakiwa wanabuluza mkia baada ya kufungwa michezo yao miwili kwa idadi kubwa ya mabao kulinganisha na Namungo.
Akizungumzia mchezo huo, Ofisa habari wa Namungo Kindamba Namlia amesema: "Kikosi chetu tayari kimeanza mazoezi tangu Jumapili, kwa ajili ya mchezo wetu ujao wa kombe la Shirikisho dhidi ya Nkana ambao tunatarajia kucheza Aprili 2, mwaka huu.
"Bado tunaamini kuwa upo uwezekano wa kufuzu katika hatua ya robo fainali licha ya kutokuwa na matokeo mazuri katika michezo yetu miwili ya kwanza ya hatua ya makundi, lakini hatuangalii yaliyopita bali tunapambana kuhakikisha tunapata matokeo mazuri katika michezo yetu minne iliyosalia,"